Samia amwakilisha Magufuli Mkutano wa SADC Swaziland

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewasili mjini Mbabane, Swaziland kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) akimwakilisha Rais John Magufuli.

Alipowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Mfalme Mswati III mjini Mbabane, Swaziland jana, Makamu wa Rais alipokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Utumishi wa Umma wa Serikali ya Swaziland, Owen Nxumalo.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo, alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake na kushuhudia vikundi mbalimbali vya burudani uwanjani hapo.

Makamu wa Rais Samia anamwakilisha Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama inayojulikana kama “SADC Double Troika” katika mkutano huo.

Leo anahudhuria Mkutano wa Wakuu na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaojulikana kama SADC Double Troika utakaojadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Falme ya Lesotho.

Mkutano huo wa SADC Double Troika utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya mkutano wa Mawaziri wa Kamati Ndogo ya Siasa na Diplomasia uliofanyika Dar es Salaam Februari 24, 2017.

Katika mkutano huo, mawaziri hao walionesha haja ya kuitishwa mkutano ili kujadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama katika nchi hizo.