Viongozi SADC wajadili viwanda, sekta binafsi

MKUTANO wa dharura wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaojadili mikakati ya jumuiya hiyo katika kuimarisha viwanda umefunguliwa jijini Mbabane nchini Swaziland huku sekta binafsi zikipewa nafasi katika utekelezaji wa mpango huo.

Katika mkutano huo uliofunguliwa jana na Mwenyekiti wa SADC Mfalme Mswati III wa Swaziland, katika ukumbi wa Grand – Lozitha, Tanzania inawakilishwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mbali ya ajenda ya viwanda, viongozi hao pia watajadili namna ya kuimarisha au kuboresha sekta za elimu, miundombinu, mtangamano wa masoko, ulinzi na usalama.

Aidha mkutano huo utajadili na kuweka mfumo wa kushirikisha sekta binafsi katika ngazi zote za utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwenye jumuiya hiyo.

Akifungua mkutano huo, Mfalme Mswati alizitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuimarisha mipango na mikakati inayolenga kuhakikisha wananchi wa nchi za jumuiya hiyo wanapata huduma bora za kijamii.

Alisema nchi wanachama wa SADC zikishirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, ana imani kuwa tatizo la uhaba wa ajira na umasikini litapungua.

Mkutano huo ulitanguliwa na mikutano ya wataalamu, Makatibu Wakuu na Mawaziri wa jumuiya hiyo.

Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Augustine Mahiga akishirikiana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Amina Salum Ali.

Katika ngazi ya Makatibu Wakuu ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Balozi Aziz Mlima ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.