Kamati za Bunge kuanza kukutana leo

KAMATI za Kudumu za Bunge zinaanza shughuli zake mjini Dodoma leo hadi Aprili 2, mwaka huu kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Saba wa Bunge Aprili 4.

Pamoja na shughuli nyingine, serikali wiki ijayo itawasilisha kwa wabunge wote mapendekezo ya serikali kuhusu mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge hivi karibuni, kamati hizo pamoja na kukutana na watendaji wa serikali katika shughuli zake pia zitatembelea maeneo mbalimbali nchini na kukagua miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa kulingana na matakwa ya kikanuni, Machi 28, mwaka huu kutakuwa na mkutano wa wabunge wote kwa ajili ya kupokea mapendekezo hayo ya serikali kuhusu mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Baada ya ziara hizo kukamilika, kamati zitachambua taarifa za utekelezaji wa bajeti za wizara inazozisimamia kwa mwaka wa fedha unaoisha kwa ajili ya kufanya ulinganisho kuhusu makadirio ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Mkutano wa Saba wa Bunge unatarajiwa kuanza Aprili 4, mwaka huu ukiwa ni mkutano kwa ajili ya kuchambua, kujadili na kupitisha bajeti za wizara mbalimbali tayari kwa utekelezaji wa shughuli za serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Aidha, hoja mbalimbali zitatolewa na wabunge kuhusu tathmini ya utekelezaji wa bajeti iliyopita ili kuboresha bajeti ijayo hasa katika maeneo ya miradi ya maendeleo.