Maktaba itakayoingiza watu 2,500 kwa mkupuo yajengwa UDSM

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani kinajenga maktaba mpya ya kisasa yenye uwezo wa kuingiza wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja pamoja na kumbi za mikutano zenye uwezo wa kuwafikia wanafunzi 600.

Ujenzi wa maktaba hiyo ni moja ya jitihada zinazofanywa na uongozi wa chuo hicho kwa ajili ya kujenga na kuboresha maeneo mbalimbali, ikiwamo pia miundombinu ya chuo hicho ambayo imekaa kwa takribani miaka 55 tangu chuo kilipojengwa.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hayo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ujenzi wa maktaba hiyo unafadhiliwa na Serikali ya Watu wa China ikigharimu fedha ya China Yuan milioni 258, sawa na Dola za Marekani zaidi ya milioni 42.

Profesa Mukandala alisema mkandarasi wa mradi huo ni Jiangsu Construction Group C. Ltd na ulianza Desemba 4, 2015 ukitarajiwa kukamilika Machi 4, 2018.

Alisema ujenzi wa maktaba hiyo chuoni hapo, umetumia eneo la mita za mraba 20,000 ambayo itatoa sura mpya chuoni hapo pindi itakapokamilika huku ikiwa pia na vifaa vya kisasa kwa ajili ya wanafunzi kusoma.

Profesa Mukandala alisema mbali na ujenzi wa miundombinu hiyo, lakini pia wameongeza ghorofa moja katika jengo la utawala kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 1.6.

Alisema mradi wa ghorofa hilo unagharamiwa na chuo hicho na ulianza Julai 18, 2014 na kukamilika Aprili mosi 2016 na halijaanza kutumika kwa kuwa utumiaji unasubiri manunuzi ya samani.

Manunuzi ya samani yanatarajiwa kukamilika mwezi huu.

Kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa mradi huo, Liang Yilian alisema ujenzi wa msingi umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa mihimili kukamilika kwa asilimia 80, ujenzi wa kuta za viambaza kukamilika kwa asilimia 50 na kazi inaendelea kulingana na ratiba ilivyopangwa.