Mabula ashangazwa na faili kutoshughulikiwa kwa miaka 23

NAIBU Waziri wa Ardhi na Maendeleo na Makazi, Anjelina Mabula amepigwa butwaa kuona faili la mwananchi wa Halmashauri ya Meru mkoani Arusha anayetaka hati miliki ya ardhi yake halijashughulikiwa kwa zaidi ya miaka 23.

Waziri Mabula aliona hayo pale alipotembelea Halmashauri ya Meru, Halmashauri ya Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha kuangalia ni kwa nini watumishi wa idara ya ardhi katika halmashauri hizo wanashindwa kuingia kwa wakati katika mfumo wa ulipaji kodi wa kielektroniki na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya shilingi bilioni 170.

Alisema inasikitisha kuona mteja anafuatilia taratibu za kutaka hati ya kiwanja kwa zaidi ya miaka 23 huku watumishi wakimzungusha kwa njoo leo ama njoo kesho au kesho kutwa.

Pamoja na Waziri huyo kuelezea kusikitishwa kwake aliuliza sababu ya faili hilo kuchukua muda mrefu lakini hakupata majibu ya msingi kutoka kwa watendaji wa idara ya ardhi wa halmashauri ya Meru.

Baada ya kushindwa kupata majibu sahihi aliagiza watumishi hao kuhakikisha wanashughulikia faili hiyo na kulitoa haraka kabla ya hatua kali za kisheria zitakazochukuliwa.

Mbali ya hilo, pia aligunduiwa mbinu chafu za watendaji wa halmashauri hizo za kuingiza baadhi ya viwanja na mashamba katika mfumo wa kielektroniki na mengine kutokuingizwa ili waweze kupiga dili na kusema tabia hiyo haitavumiliwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, Waziri Mabula alitoa muda hadi Juni 30 mwaka huu halmashauri hizo ziwe zimewepa wale wote waliomba hati na na kuonesha idadi ya viwanja na mashamba yote katika mfumo huu, ili wizarani iwe rahisi kufuatilia nani amelipa kodi na nani hakulipa kodi.