Walima tumbaku wafurahishwa na uamuzi wa Waziri Mkuu

WAKULIMA wa tumbaku kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora wamefurahishwa na uamuzi wa kutimuliwa viongozi wote wa Chama Kikuu Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) uliochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Hatua hiyo imetokana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasimamisha viongozi wa Bodi ya Wetcu na uongozi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) yenye dhamana ya kusimamia zao hilo nchini, mwishoni mwa wiki alipozuru mkoani hapa.

Wakulima hao wamesema umaskini walio nao umechangiwa na viongozi wa bodi hiyo kwani walishindwa kabisa kusimamia maslahi yao huku wakijijali wao wenyewe kwa kulipana posho nene za jasho la wakulima hao.

Wamesema mpaka sasa wanaidai bodi hiyo mabilioni ya fedha zikiwa ni sehemu ya malipo yatokanayo na mauzo ya tumbaku yao na hapakuwa na wakati wowote wa kulipa fedha hizo kwa wakati huku wakulima wakiendelea kukatwa madeni ya pembejeo.

Mkulima wa Kijiji cha Mole wilayani Sikonge ambaye aliomba asitaje jina gazetini, alipongeza uamuzi huo kwani viongozi hao walikuwa wabinafsi na kujifanya miungu watu hali iliyopelekea kulundikana kwa madeni yao.

Mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Jilala kutoka wilayani Kaliua, alisema Wetcu walikuwa wajanjawajanja ndio maana hata vikao vya mkutano mkuu wa wakulima wa zao hilo vilikuwa vikitaliwa na mwenyekiti pekee na hawakuwa tayari kukoselewa.

Mwenyekiti wa Wakulima Binafsi wilayani Kaliua, Morris Rubundi ambaye ni mkulima na mkazi wa Usinge alipongeza hatua iliyochukuliwa na serikali kwa kuwa Wetcu iliwaonea sana na ilikuwa haiwatendei haki.

Alisema kitendo cha baadhi ya wakulima kuamua kujitenga na ushirika huo kilisababishwa na viongozi hao kutumia fedha zao vibaya na kushindwa kusimamia ipasavyo maslahi ya wakulima wote huku wakinemeeka kwa jasho la wakulima.

“Uamuzi wa kuvunjwa kwa Bodi ya Wetcu na uongozi mzima wa Bodi ya Tumbaku (TTB) hapa nchini umetufurahisha sana, sasa tutapumua, tunaomba serikali itusaidie kupata masoko ya kuuzia tumbaku yetu ya msimu wa 2016/17,” aliongeza.

Mbali na kuvunjwa kwa Bodi ya Wetcu na ile ya TTB ikiwemo kutenguliwa kwa uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Vita Kawawa, Waziri Mkuu Majaliwa alitangaza kusimamishwa kwa shughuli zote za Wetcu mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Aidha, alimuagiza mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji, maofisa kilimo na ushirika na watendaji wote wa serikali katika mkoa huo kuacha tabia ya kukaa maofisini bali wakasimamie ipasavyo kilimo cha zao hilo na kutatua kero zote za wakulima.

Alionya tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali katika mikoa na wilaya kufanya mzaha katika mambo ya msingi yanayohusu maisha ya wananchi kwa kushindwa kuchukua hatua haraka pale wanapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo.

Aliwataka maofisa kilimo na ushirika kwenda kwa wakulima na kuwapa elimu ya kilimo bora huku akiwaagiza kuweka utaratibu mzuri utakaowawezesha kujitegemea ili kuepuka utegemezi wa mikopo ya mabenki kila msimu.