ACT waanza uteuzi wagombea ubunge Afrika Mashariki

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeanza uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ndani ya chama hicho na kutangaza mwisho wa kurudisha fomu itakuwa kesho saa 10:00 jioni.

Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alisema uteuzi wa wagombea hao ulianza juzi Machi 18 na fomu za wagombea zilianza kutolewa jana.

“Kama mnavyofahamu tayari mchakato wa kuwapata wabunge watakaowakilisha nchi EALA sisi ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo baada ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mtemelwa.

Alisema, “ACT Wazalendo kitawapatia Watanzania watu walio bora na makini watakaoenda kuiwakilisha nchi ndani ya jumuiya hiyo na tuna uhakika wa wagombea watakaoteuliwa na chama chetu watakuwa makini na hodari wa kujenga hoja kabla ya kuwa wabunge na baada ya kuwa wabunge.”

Aidha, alisema Machi 25, mwaka huu watafanya Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia jijini Arusha unaofanyika kila mwaka ambao huwashirikisha wanachama wote na wasio wanachama huku ukiwa hauna wajumbe mahususi na unajikita zaidi katika kujadili masuala ya maendeleo ya nchi na dunia kwa ujumla.

Alisema maandalizi ya mkutano huo yameshakamiliki kwa asilimia zaidi ya tisini na kutakuwa na mijadala mbali mbali kutoka kwa wawakilishi wa taasisi za ndani na nje ya nchi ambapo alitoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kuhudhuria mkutano huu na kujadiliana masuala tofauti kwa ajili ya nchi.

Pia alimuomba Rais John Magufuli kuendelea na mchakato wa kuwapatia Watanzania wanyonge Katiba mpya itakayotoa nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotekeleza wajibu wao kulingana na nafasi walizo nazo.