Sera ya misitu kupitiwa upya

WIZARA ya Maliasili na Utalii (Idara ya Uendelezaji Ufugaji Nyuki) ina mpango wa kuipitia Sera ya Misitu ili kuona ni kwa namna gani inaweza kushirikisha wadau wa sekta binafsi pamoja na masuala mbalimbali ambayo wanafikiri yanaweza kuleta manufaa katika eneo hilo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji , Ufugaji Nyuki katika wizara hiyo, Allen Richard alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati Ubalozi wa Finland ulipokuwa ukitoa msaada wa fedha kwa kampuni binafsi zinazojishughulisha na kupanda miti, lengo likiwa ni kuimarisha utunzaji wa mazingira.

Kuhusu Sera ya Misitu, Richard alisema wizara hiyo ina mpango wa kuipitia, wakitarajia pia kuwaita wadau ili kuona ni kwa namna gani sekta hiyo inaweza kuzungumzia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika eneo la mazingira.

“Sera hiyo inaweza kukamilika hivi karibuni na itakuwa na kile ambacho wadau wanahitaji kiwepo ili kupambana na changamoto za mazingira,” alifafanua na kuongeza kuwa yamekuwepo mahitaji makubwa ya mbao jambo ambalo kupitia sera hiyo serikali itahamasisha jamii kupanda miti kwa wingi na kutojihusisha na uvunaji haramu.

Hata hivyo, alisema serikali ina mpango wa kupanda miti nchini kote kwa kufikia hekta 185,000 katika mwaka huu wa fedha, ikiwa ni mpango mkakati wa miaka 10.