Wakulima washawishiwa kujenga maghala kukwepa walanguzi

WAKULIMA wadogo wameshauriwa kuzingatia umuhimu wa kujenga maghala ili kuepuka ulanguzi wa bei unaofanywa na wanunuzi wa mazao wasio waaminifu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Mfuko Kichocheo wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOTCTF), Dk John Kyaruzi wakati akizungumza na wakulima katika Kongamano la mwaka la wabia na wadau wa SAGCOT 2017 jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Dk Kyaruzi alismea maghala yatasaidia kuwaepusha na walanguzi wa bei ya mazao yao.

“Maghala husaidia kuhifadhi mazao wakati wakiendelea kuzungumza na wanunuzi kuhusiana na bei nzuri ya sokoni, hivyo miongoni mwa changamoto tunazozitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ni ujenzi wa maghala,” alisema.

Alisema changamoto kubwa za wakulima wadogo hawana vikundi imara vinavyoweza kuingia mikataba ya kuheshimika, pili kutoona umuhimu wa maghala kama sehemu ya biashara.

Mfumo wa soko ikiwemo bei nzuri. Tunawashauri wawekeze kwenye maghala kwa sababu ndiyo sehemu sahihi ya kuhifadhi mazao wakati wakisubiri bei bora,” alisema Dk Kyaruzi.

Alitaja changamoto nyingine ya kuwapatia wakulima fedha kwa ajili ya kuendeleza kilimo kwani kuna wakulima wa aina mbalimbali, mkulima mdogo hawezi kukopesheka, kikubwa kinachofanya ni kumlea kwa kumwongoza alime kibiashara badala ya kukupa fedha.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya SAGCOT CTF na Katibu Mkuu Wizara mstaafu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mbogo Futakamba alisema suala wanalotilia mkazo kwa sasa ni ujenzi wa viwanda ili wakulima wadogo wapate soko la uhakika.