Wakurugenzi waagizwa kusaka fedha kukamilisha mradi wa maji

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge amewapa siku tatu wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Dk Oscar Mbyuzi na wa Wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito kutafuta fedha zitakazokamilisha mradi mkubwa wa maji katika Kijiji cha Ukuli, Kata ya Kingilikiti wilayani Nyasa.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2012 na kukaguliwa na mkuu huyo wa mkoa akiwa Naibu Waziri wa Maji, hadi sasa ni miaka mitano haujakamilika na wananchi wa kijiji hicho wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji.

Dk Mahenge alisema Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa na dhamira kubwa ya kuwaondolea wananchi kero ya maji, lakini jambo la kushangaza bado kuna watu ambao wamekwamisha kukamilika kwa mradi huo licha ya kutengewa fedha nyingi ambazo zingetosheleza kumaliza ujenzi wake.

“Viongozi wenzangu niwaambie tu ukweli, katika mradi ule wa maji tunalo deni kubwa kwa wananchi wa Kata ya Kingilikiti, ule mradi ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2012 mimi nikiwa Naibu Waziri wa Maji na nilipata fursa ya kuukagua lakini nimeumia sana kuona hadi leo bado haujakamilika,” alisema Dk Mahenge.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Evaristo Ngole akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, alisema mradi huo ulitekelezwa kwa awamu mbili; ya kwanza ulisainiwa mwaka 2012 na ulihusisha ukarabati wa chanzo cha maji ambacho kipo Kijiji cha Buruma wilayani Mbinga.

Alisema hata hivyo mkandarasi wa kwanza Kampuni ya M/S Kipera hakumaliza kazi ya mkataba na serikali ililazimika kumtafuta mkandarasi mwingine, Kampuni ya Interplan ambaye baada ya kukamilisha kazi ya kufunga mabomba wakati wa majaribio ya kupeleka maji kwenye tangi, ilijitokeza shida ya bomba kuachia kwenye viunga na kukwamisha kuanza kwa huduma ya kupatikana kwa maji hadi sasa.