Pori tengefu Loliondo lina vita ya maslahi-RC

VITA ya kimaslahi inayotokana na utalii, ushindani wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) pamoja na masuala ya siasa kuingizwa katika utatuzi wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo vinasababisha baadhi ya wananchi wa kata saba wilayani hapo kufikiria wanaporwa ardhi ya kilometa za mraba 1,500 imebainishwa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amekerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa jamii pamoja na baadhi ya madiwani kushawishi wananchi kufunga barabara na kuwapiga wataalamu wa ardhi wanaofanya kazi ya kuweka alama za mipaka kwenye maeneo ambayo ni muhimu kwa ajili ya malisho, wanyamapori pamoja na utalii.

Hayo yalibainika wakati kamati hiyo ikiongozwa na RC Gambo pamoja na timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali ambapo ilipokumbana na maandamano katika Kata ya Oloipiri ambapo wananchi hao ambao asilimia kubwa wametangulizwa mbele ni kinamama na watoto wadogo waliodai ardhi yao kuchukuliwa na serikali.

“Nimegundua huu mchezo mnaoufanya: lazima kuna watu ndani yake aliyewaambia nani kuwa serikali inachukua ardhi hii hivi nyie viongozi ambao mpo ndani ya Tume hii kwa nini mnawaingiza wananchi katika vita ya Mwarabu na Mmarekani?

Na mnapodai eti miongoni mwenu hakuna Wakenya mnadhani serikali haijui, sasa baada ya zoezi hili DC, Taka anzisha msako wa kubaini wananchi ambao si raia wa Tanzania maana sasa nyie mnafanya mchezo na serikali, na wanaowachochea kuhusu mgogoro huu tutawakamata,” alieleza mkuu wa mkoa.

Alisema ni kweli Wilaya ya Ngorongoro kuna watu ambao si raia wa Tanzania wanaishi hapo na endapo jamii hiyo ya Wamasai ikiendelea kuwahifadhi, serikali haitawavumilia hata kidogo na kisha alimwagiza DC wa wilaya hiyo, Rashid Taka kuhakikisha anafanya msako mara baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake ili kubaini raia wakigeni wanaoishi kinyemela.

Pia alisisitiza kuwa ni vyema sasa kampuni ya Endboyond kufahamu kuwa serikali ipo na inapaswa kuitambua Wizara ya Maliasili na Utalii kama vile Kampuni ya OBC inavyoitambua wizara hiyo na kulipa kodi serikalini na kuwasisitiza wananchi kuacha kutumika kwa kitu wasichokijua juu ya mgogoro huo wa Pori Tengefu la Loliondo.

Tume hiyo inatarajia kuwasilisha ripoti yake Machi 25, kwa Waziri Mkuu, Majaliwa ambayo aliagiza tume hiyo kufanya kazi yake ili kutatua mgogoro huo uliodumu kwa miaka 25 sasa.