Wazee wampongeza Rais Magufuli kwa kuwajali

JUMUIYA ya Baraza Huru la Wazee katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma limempongeza Rais John Magufuli kwa hatua mbalimbali alizochukua zinazolenga kuboresha maisha ya wazee nchini.

Wakizungumza katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge mjini hapa, walisema tangu Dk Magufuli aingie madarakani miaka miwili iliyopita, wameonesha tofauti kubwa hasa baada ya kuanzisha wizara inayohusika na kusimamia mambo ya wazee na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wazee nchini.

Walisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake ameonesha dhamira ya kweli kwa kila jambo analosema kwa wananchi na kutolea mfano kusimamia tatizo la watumishi hewa, ufisadi kwa watumishi wa umma, kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

Aidha, wazee hao wamesema Dk Magufuli ni mfano mzuri wa kuigwa na watumishi wote wa umma kuanzia nagzi ya chini kwa kila mara ameonekana kufanya kazi nzuri kwa maslahi ya walio wengi badala ya kutanguliza maslahi binafsi.