Wanawake Moro wapanda miti kurejesha uoto

WANAWAKE kutoka katika kata 29 za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wamejitokeza katika kampeni ya upandaji miti kando kando ya bwawa la Mindu ili kuzuia uharibifu wa mazingira.

Kampeni hiyo imeanzishwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Devota Minja, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alisema kwa kuanzia wamepanda miti 600.

Akizungumza na gazeti hili, Minja alisema ameanzisha kampeni hiyo kutokana na kuwepo kwa tatizo la maji katika mji wa Morogoro na wilaya zake linalosababishwa na uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.

Alisema kampeni hiyo aliizindua kwenye maadhimisho ya Wiki ya Maji ambapo miti 6,000 inatarajiwa kupandwa katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro.

Alisema lengo jingine la kampeni hiyo ni kutaka kurudisha mandhari ya Morogoro hasa manispaa ilivyokuwa miaka ya 1970 hadi 1980 wakati Milima ya Uluguru ilipokuwa imefunikwa na uoto wa asili na maji yalikuwa yakitiririka mwaka mzima.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa wa Maji Bonde la Wami Ruvu, Grace Chitanda alisema mito mingi inayoingiza maji kwenye Bwawa la Mindu imepoteza mkondo wake na mingine haipeleki maji kutokana na shughuli za kibinadamu za kilimo, uchepushaji maji, ufyatuaji matofali, uchimbaji mchanga na ukataji miti.

Chitanda alisema Ofisi ya Bonde la Wami Ruvu inafanya jitihada za kufukua mito yote inayoingiza maji kwenye bwawa hilo ambalo linategemewa na asilimia 75 ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro.