Tanga Uwasa wafundisha matumizi lazima ya maji

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) imewataka wateja wake kuwa waangalifu katika matumizi ya majisafi hata kama wana uwezo wa kuyalipia na kuhakikisha wanajiwekea utaratibu mzuri wa kuyatumia kwa ufanisi ili kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.

Utekelezaji wa hatua hiyo pamoja na mambo mengine utasaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimali maji pamoja na vyanzo vya uhakika vya maji ambao umeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa, Joshua Mgeyekwa ametoa mwito huo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Maji 2017 ambao umekwenda sanjari na kutoa elimu kwa wanahabari wa mkoani humo kuhusu matumizi ya Mkataba wa Huduma kwa Mteja.

Mgeyekwa alisema lengo la maadhimisho hayo ambayo hufanyika kati ya Machi 16 na 22 kila mwaka ni kuwashirikisha wananchi na wadau wa Tanga Uwasa katika kutathmini mafanikio, chanagamoto na kutoa maoni ili kubadilishana uzoefu utakaoboresha utoaji endelevu wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.

“Ili kuwezesha rasilimali maji kuwa endelevu inampasa kila mwananchi kuwa makini na mwangalifu katika matumizi kwa kukazia matumizi ya lazima tu, huku akijitahidi kupunguza matumizi pale inapobidi ili kuruhusu yatumike kwa shughuli nyingine za uzalishaji tofauti na ilivyo hivi sasa,” alisema Mgeyekwa.

Akizungumzia huduma ya majitaka, alisema ni vema wateja wakaanza kufikiria namna kutumia kama fursa ya kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji kiuchumi.

“Kwa kuwa mpaka sasa hatuna mfumo wa kusafisha majitaka kabla ya kuyamwaga baharini, mamlaka imetenga eneo maalumu la kujenga mabwawa ya majitaka katika eneo la Utofu kwa ajili ya kuwezesha baadhi ya wakazi kufanya kilimo cha matunda, mboga za majani pamoja na kufuga samaki ili kupanua wigo wa matumizi ya raslimali maji kwa kujiongezea kipato,” aliongeza mtendaji huyo.

Alisema katika maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu isemayo ‘Majisafi na Majitaka Punguza Uchafuzi Yatumike kwa Ufanisi.”

Tanga Uwasa itafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wakazi kujiunga na mfumo wa majitaka, kutoa msamaha wa tozo la kurejesha huduma kwa wateja waliositishiwa pamoja na kuyaelimisha makundi kadhaa ya wateja matumizi ya Mkataba wa Huduma kwa Mteja ili kuongeza tija.