Watakaokataa kuchangia chakula kukamatwa

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge ametangaza kuwa wataanza kuwakamata na kuwachukulia hatua wazazi na walezi wanaokataa kuchangia chakula cha mchana mashuleni kwa ajili ya watoto wao kwani inasikitisha kuona baadhi ya shule hazitoa chakula hicho licha ya mkoa kubarikiwa kupata mavuno mengi kila mwaka.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba watoto wao wanakwenda shule na kutumia fursa ya elimu bure iliyotangwaza na Rais John Magufuli kusoma vizuri ili wapate elimu itakayowasaidia kutimiza ndoto zao.

Dk Mahenge ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha pamoja kati ya mkuu wa wilaya na baadhi ya wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wake, mzazi au mlezi atakayeshindwa kuchangia chakula cha mchana atahesabika ni mwizi kwa sababu katika mazingira ya kawaida ya Mkoa wa Ruvuma wenye ardhi kubwa na yenye rutuba unaopata mvua za kutosha kila msimu, kitendo cha kusema mtuj hana cha kuchangia ni dalili ya wizi.

Mbali na kuhimiza uchangiaji wa chakula shuleni, Dk Mahenge ameagiza kila mzazi mwenye mtoto shuleni ahakikishe ananunua sare na baadhi ya mahitaji muhimu kwa mtoto badala ya kusubiri kila jambo kufanywa na serikali.

Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye pamoja na watendaji wengine wilayani hapa kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mafanikio ya maendeleo kwa kusimamia vizuri fedha za miradi kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na kutekeleza miradi ya maendeleo.