Sababu za Mbeya kukumbwa na vifo, Ukimwi zatajwa

UWEPO wa barabara kuu za kwenda nchi jirani za Zambia na Malawi, njia ya reli ya Tazara na mazao mengi ya chakula na biashara, umetajwa kuwa chanzo kikubwa cha Mkoa wa Mbeya kuwa kwenye hatari zaidi ya ya ongezeko ya vifo vya akina mama na watoto wachanga sanjari na kukumbwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja alibainisha hayo alipofungua Tamasha la Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Marie Stopes Tanzania na kufanyika kwenye Viwanja vya Soko la Kimataifa la Mwanjelwa jijini hapa.

Mtunguja alisema Mkoa wa Mbeya uko katika hatari hiyo ya Ukimwi kutokana na kupitiwa na barabara kuu ambayo inapokea wageni wengi hivyo wakati wa mapumziko wanatumia muda mwingi kuwarubuni vijana hususani wasichana na hatimaye kuwaambukiza VVU na kuwapa mimba katika umri mdogo.

“Si barabara kuu pekee, hapa kwetu tumepitiwa na Reli ya Tazara, lakini pia tuna fursa kubwa ya uzalishaji mazao hivyo wageni wengi wanakuja kununua mazao mkoani kwetu. Hizi zote ni changamoto zinazotufanya tuwe kwenye hatari zaidi ya mimba za utotoni na maambukizi ya VVU,” alifafanua Mtunguja.

Alisema katika utafiti uliofanyika hivi karibuni, ulibaini kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 Tanzania, asilimia 3.3 wameathirika ilhali Mkoa wa Mbeya pekee ni asilimia 6.3 hali inayoashiria mkoa kuwa katika hatari zaidi ya kuwa na maambukizi kwa vijana wadogo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Mbeya, Prisca Butuyuyu alisema katika utafiti wa mwaka 2010, zaidi ya asilimia 23 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 walipata mimba, lakini mwaka 2015 idadi iliongezeka na kufikia asilimia 27.

Butuyuyu alisema mwaka 2016, Mkoa wa Mbeya pekee uliripotiwa kuwa na vifo 94 vya wajawazito na kati yao 27 sawa na asilimia 31 walikuwa ni wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 vifo ambavyo vilisababishwa na kupungukiwa damu, kifafa cha mimba, maralia na vichomi.

Alisema visababishi vya vifo hivyo kwa vijana ni kutokana na aibu hivyo wengi kuficha mimba na kusababisha kukosekana kwa huduma na wengine kukimbilia kutoa bila kutumia njia sahihi hivyo kupelekea kupoteza maisha.

Naye Mratibu wa Vijana kutoka Marie Stopes, Daniel Emmanuel alisema lengo la tamasha hilo lililowakutanisha wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari na vyuo, ni kuwafikia vijana wengi ili kuwapa elimu ya afya ya uzazi, ushauri kuhusu maambukizi ya Ukimwi na ukatili wa kijinsia.

Emmanuel alisema walengwa hasa wa mpango huo ni vijana wote walioko katika shule za sekondari, vyuoni na wanaojishughulisha na biashara mbalimbali walio na umri kati ya miaka 15 hadi 24 kwa kuwa ni kundi lililo kwenye hatari zaidi ya kukumbwa na mimba za utotoni na maambukizi ya Virusi Vvya Ukimwi.