Jenista ashangaa uamuzi wa Kafumu, Kamata

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk Dalaly Kafumu na Makamu wake, Vicky Kamata wamejiuzulu nafasi zao kwa hofu ya kupoteza ubunge 2020 pamoja na kupata ushirikiano hafifu wa serikali na baadhi ya wabunge.

Pia wamesema kwa nyakati tofauti kuwa kumekuwa na ushirikiano usio na tija baina ya kamati wanayoingoza, serikali na baadhi ya wabunge wa CCM na upinzani, kupinga hoja zenye mashiko kwa nchi.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu, Jenista Mhagama alionesha kushangazwa na uamuzi huo ambapo alisema hakuna mahali ameona serikali haisikii wala kuchukua ushauri wa kamati yoyote.

“Ninachojua shughuli za Bunge zinafuata kanuni na taratibu, mijadala hufanyika ndani ya Bunge na kamati zinaishahuri serikali kwa mujibu wa hizo kanuni. Serikali huleta taarifa bungeni, miswada huwasilishwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu,” alifafanua Jenista.

Alisema serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17- 2020/21) kwa njia ya Mpango wa mwaka mmoja mmoja, na mambo mengi yanafanyiwa kazi kwa ushauri na maboresho ya kamati za Bunge na kusisitiza kuwa, wakati wote Serikali itaendelea kupokea ushauri kwa maslahi ya nchi Kuhusu uelewa wa viongozi na kamati kuhusu dhana ya Tanzania ya viwanda kuwa mdogo kama alivyoeleza Dk Kafumu alipozungumza na waandishi.

Waziri Jenista alisema ni vizuri kuweka wazi aina ya viongozi wenye uelewa duni kwa kuwa nchi ina viongozi kuanzia ngazi za vijiji hadi taifa.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Dk Kafumu ambaye ni Mbunge wa Igunga mkoani Tabora (CCM) na Kamata ambaye sasa anajitambulisha kuwa ni Vicky Likwelile ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita (CCM), walisema kuwa hawajashinikizwa na mtu bali uamuzi huo ni kwa manufaa ya nchi na yao kisiasa.

“Nakosa muda wa kukaa jimboni na vikao vya kamati ya fedha jimboni vinanipita, nimekosa nafasi ya wananchi wangu. Hii imenifanya nitazame upya nafasi yangu kama mwenyekiti wa kamati hii. Naacha nafasi ya uenyekiti. “Nimezungumza na Spika, napeleka barua ya kuacha nafasi hii kwake, miaka miwili imebaki kutumikia vizuri jimbo langu,” alisema Dk Kafumu ambaye amekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo kwa zaidi ya mwaka sasa.

Dk Kafumu alisema pamoja na hilo wapo vijana wanapitapita jimboni kwake kwa kasi hivyo ana hofu ya kupoteza jimbo mwaka 2020 kutokana na kubanwa na kazi za kamati ndani na nje ya nchi zaidi ya jimboni kwake, hivyo anataka kuhamishia nguvu jimboni.

Akifafanua zaidi, Dk Kafumu alisema pamoja na hoja hiyo ya jimboni ambayo ndio alisema ni ya msingi kwake kuachia nafasi hiyo, lakini alieleza kuwa kumekuwa na ushirikiano hafifu baina ya kamati, serikali na baadhi ya wabunge wakiwemo wa CCM kupinga hata mambo ambayo yana tija kwa taifa kuelekea nchi ya viwanda.

“Ukifanya jambo la serikali, mbunge wa CCM analipinga. Labda kazi hii ni kubwa kuliko uwezo wetu, ukishauri jambo halifanyiwi kazi, acha wengine waendelee,” alisema Dk Kafumu, mtaalamu wa masuala ya madini aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini nchini.

Alisema walishauri kuhusu maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na wamefanya tathimini na kuandika taarifa nzuri ya kamati namna ya kuishauri serikali, ila wanaona kuna mvutano kufanyia kazi mapendekezo yao hivyo wanaona nafasi zao wachukue wengine ili mambo yaende.

Dk Kafumu alisema tayari alishazungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu uamuzi wake na ingawa alionesha kutokubali, lakini baadaye aliwaelewa na kukubaliana na uamuzi wao na jana walipeleka barua ya kujiuzulu kwake (Spika). Naye Kamata alisema, “Nami najiuzulu nitoe nafasi kwa wabunge wengine wafanye kazi hii.”

Alisisitiza kuwa amewaacha muda mrefu wanawake wa Geita na hasa taasisi yake ya Victoria Foundation kwa kukosa muda kushughulika na mambo yao kwa kubanwa na shughuli za kamati.

Kauli ya Spika Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya Kamata na Dk Kafumu kupeleka barua zao ofisini kwake, Spika Ndugai alisema hajapokea barua hizo na kwamba akipokea atakuwa na nafasi nzuri ya kuzungumza.

Hata hivyo, baadaye jioni, ofisi yake ilipokea barua hizo. Mjumbe wa Kamati azungumza Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (CCM) alisema ni pigo kubwa kwao kwani Dk Kafumu aliwaeleza jana asubuhi msimamo wake wa kuiuzulu wakati akizungumza na kamati kuhusu shughuli za kamati kuanza rasmi.

Nyongo alisema wajumbe wamejitahidi kumuomba Dk Kafumu aghairi msimamo wake, lakini inaonekana alishaamua na hivyo hawawezi kuwalazimisha ingawa kwao ni pigo kubwa.

“Dk Kafumu ana uzoefu mkubwa, miaka 30 serikalini, anajua mambo mengi na alikuwa akituelimisha mengi. Hakuna namna, wataendelea kuwa wajumbe. Katika uongozi wao kamati imefanya mengi, ushauri wa maboresho bandarini tunakumbuka hata Rais wa Congo (DRC), Joseph Kabila alikuja nchini na wafanyabiashara wa Congo wamerejea kutumia bandari yetu,” alieleza Nyongo.

Ushauri wao kwa serikali Dk Kafumu alishauri kuwepo na mkakati wa pamoja na serikali kuhakikisha nchi inafika kuwa ya viwanda hasa kwa kuweka masuala yote ya uwekezaji yakiwa katika sehemu moja badala ya ilivyo sasa kila mamlaka na idara husika ina utaratibu wake jambo linalochelewesha nchi kufikia uchumi wa kati.

“Sasa hivi mwekezaji atatakiwa kwenda Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) huko atapewa kibali, atapaswa apate ardhi lazima aende wizara husika, atapaswa kwenda wizara ya viwanda, anakata tamaa, inafaa apate vyote hivi pamoja kama wanavyofanya Kenya, Rwanda na Uganda,” alishauri Dk Kafumu.

Dk Kafumu alisema kunahitajika mtazamo wa pamoja na si wa mtu binafsi kuhusu Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kubainisha kwamba uelewa wa viongozi na wananchi kuhusu nchi kua ya viwanda si mkubwa hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuweka ajenda hiyo.

Kauli ya Serikali Akizungumzia na gazeti hili kwa simu kuhusu ushauri wa kamati hiyo katika masuala ya bandari, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mara zote wizara yake imekuwa ikipokea ushauri wa kamati na Mtanzania yeyote kuhusu maboreshi ya sekta inayozisimamia.

“Mara zote sisi kama serikali tunapopata maoni ya kamati na Mtanzania yeyote tunapokea na kuyafanyia kazi. Huwezi kufanya kazi peke yako lakini kuna mapendekezo na maboresho huwezi kuyafanya overnight (kwa usiku mmoja). “Project (miradi) nyingine zinahitaji miaka mitatu. Vyote vinafanyika kwa maslahi ya Taifa. Serikali imekuwa ikisikiliza kamati kwa maslahi ya nchi na mtu yeyote mwenye maoni, wazo, mapendekezo ofisi yetu ipo wazi,” alisisitiza Profesa Mbarawa.

Utaratibu Mwenyekiti na Makamu wakijiuzulu Utararibu wa kikanuni inapotokea mwenyekiti na makamu wake wakijiuzulu nafasi zao mamlaka ya kufanya uchaguzi mwingine ipo mikononi mwa kamati husika. Kamati inaweza kuchagua viongozi wa muda ama viongozi wa kudumu kwa namna wanavyoona inafaa.