Magufuli: Tanzania kuwa mfano Afrika

RAIS John Magufuli ametaja orodha ya miradi inayotekelezwa na serikali yake ambayo itabadilisha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam na kupunguza msongamano wa magari na ambayo itaifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano barani Afrika katika kujiletea maendeleo.

Akizungumza jana wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za mapishano ya juu inayojengwa kwenye makutano ya barabara ya Mandela na Morogoro, Rais Magufuli aliutaja mradi huo kuwa ni mradi mkubwa kutekelezwa nchini ambao pamoja na kusaidia kupunguza tatizo la msongamano wa magari, lakini utaleta sura mpya kwa Jiji la Dar es Salaam.

“Huu ni mradi mkubwa na wa aina yake, wa kwanza kutekelezwa hapa nchini. Tunataka kama sio kumaliza basi upunguze tatizo la msongamano, lakini pia utaboresha mandhari ya jiji letu ambalo linakuwa kwa kasi,” alisema Rais Magufuli.

Mradi mwingine ambao alisema utapunguza msongamano ni ujenzi wa barabara za ghorofa unaoendelea kujengwa katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela.

Mradi huo unajengwa na kampuni ya ujenzi kutoka Japan. Alisema ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam-Bagamoyo hadi Msata imekamilika na itazinduliwa hivi karibuni.

Alisema malori na mabasi ya kwenda mikoa ya kaskazini na nchi jirani hayana haja ya kupita barabara ya Mandela sasa wanaweza kutumia barabara hiyo na hivyo kupunguza msongamano.

Aliongeza kuwa ujenzi wa bandari kavu unaoendelea eneo la Ruvu utasaidia mizigo yote inayoenda nchi jirani na mikoani kuchukuliwa na magari makubwa katika eneo hilo.

Alisema Benki ya Dunia imekubali kutoa dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya kuboresha ukarabati wa reli ya kutoka bandarini hadi Ruvu, hivyo malori hayatalazimika kufika Dar es Salaam, hali ambayo itapunguza msongamano mkubwa wa magari uliopo sasa.

Alisema serikali iko kwenye hatua za mwisho za kujenga njia sita ya kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ambayo itajengwa kwa ubia na sekta binafsi.

Alisema ujenzi wa awamu ya pili na tatu ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), fedha zake zitatolewa na Benki ya Dunia nazo zitasaidia kupunguza msongamano.

Alisema ujenzi wa daraja kutoka Hospitali ya Aga Khan kwenda Coco Beach uko mbioni kukamilika. Aliongeza kuwa kwa sasa wanatafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara za ghorofa katika makutano ya Mwenge, Morocco, Magomeni na Tabata.

“Pia tumetenga shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kuweka lami katika barabara za mzunguko za Da res Salaam ambazo tunaamini zitasaidia kupunguza msongamano wa magari,” alisema Dk Magufuli na kutaja ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kuwa nao utasaidia katika aeneo hilo.

Mikopo ya Benki ya Dunia

Mradi uliowekewa jiwe la msingi jana una urefu wa kilometa moja, unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia ambazo ni Sh bilioni 186.72.

Fedha hizo ndizo zitatumika kujengea mradi huo na ndizo zimetumika pia kufanyia upembuzi na usafiri wa mradi huo. Serikali imetoa Sh bilioni 1.98 kwa ajili ya kuwalipa fidia watu ambao wataathiriwa na mradi huo.

Alisema huo sio mradi wa kwanza kutekelezwa na benki ya dunia hapa nchini, kwani benki hiyo kwa sasa inatekeleza miradi mingine 28.

Baadhi ya miradi hiyo ni uboreshaji wa reli, mahakama, usambazaji wa umeme vijijini, vyuo vikuu vya Sokoine na Mandela na uboreshaji wa elimu ya msingi.

Alitaja miradi mingine kuwa ni uboreshaji wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi awamu ya pili na tatu, usambazaji wa maji safi na maji taka, kuboreha miji ya Arusha, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Mtwara.

Alisema miradi yote hiyo inatekelezwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 780 (sawa na Sh trilioni 1.74).

Aliongeza kuwa licha ya mkopo huo, Benki ya Dunia pia imekubali kutoa mkopo wa dola za Marekani milioni 1,284 (sawa na Sh trilioni 2.79) ambazo zitaenda kwa miradi ya upanuzi wa bandari, uboreshaji wa mifumo ya umeme ya Tanesco, Uboreshaji wa umeme wa gesi, sekta ya elimu, elimu ya juu, sekta ya afya na Zanzibar.

“Tanzania sisi ni matajiri ndio maana tunaaminiwa hadi kukopeshwa, benki ya dunia endeleeni kutuamini na nakuhakikishia kwamba mikopo yote tutailipa,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa fedha zote zitatumika kwa matumizi yaliyopangwa na hakuna mtu atakayekula hata senti 5, kwani atakayefanya hivyo atatumbuliwa.

Ujenzi kukamilika haraka

Rais Magufuli alisema kwa kuwa fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za ghorofa za makutano ya Ubungo zipo, haona sababu ya ujenzi kuchukua miezi 30.

Alishauri kama inaawezekana ujenzi wa mradi huo uchukue miezi 20 tu.

Alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha anamsimamia mkandarasi ambayo ni Kampuni ya CCECC ya China kuhakikisha anajenga barabara hiyo mchana na usiku.

“Hakuna sheria inayozuia ujenzi nyakati za usiku, tena kujenga usiku ni nzuri zaidi maana hakuna msongamano wa magari,” aliongeza Dk Magufuli.

Alisema ni jambo jema kwamba mkandarasi akimaliza haraka analipwa fedha zake kwa haraka, kwani Watanzania wanataka kuona mradi huo unaisha haraka pia.

Hata hivyo amewaagiza Watanzania kulipa kodi, ili Serikali iweze kupata fedha za kulipa mikopo hiyo na za kufanyia maendeleo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird walitia saini ya mikataba mitatu.

Mikataba hiyo ni utoaji wa fedha kwa ajili ya kuboresha usafiri jijini Dar es Salaam, Uboreshaji wa sekta ya maji na kuboresha baadhi ya miji nchini.

Kupoteza muda

Rais pia aliwataka Watanzania kuzungumzia masuala ya maendeleo na kuacha kutumia muda mwingi kwa mambo ambayo hayana manufaa katika maisha yao.

Alishangaa Watanzamia kwamba wamejielekeza kwenye mambo ya kuzungumzia watu badala ya mambo ya kuwaletea maendeleo.

Alisema hayo mambo hayawasaidii hata kupata fedha za kuwapeleka watoto wao shule, lakini ndio wanayotumia muda mwingi kuyajadili.

“Nashangaa mnachukua muda mwingi kwa mambo ambayo hayawasaidii hata kuongeza dawa huko hospitalini...na wengine wanataka hata kuingilia uhuru wangu juu ya nani nimteue...mimi sipangiwi...mimi sioneshwi njia ya kupita,” alieleza Rais Magufuli. Alisema yeye hapangiwi na mtu nini cha kufanya.

Alisema mtu akishampangia hawezi kuchukua hatua kwa kuwa tu watu wanataka iwe hivyo.

“Mimi kwangu ukinipangia na ukaniingilia uhuru wangu, hapo umepoteza, siwezi kupangiwa na mtu,” alifafanua.

Aliongeza kuwa hakuna mtu aliyempangia hata alipoamua kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais, aliamua mwenyewe bila kushauriwa na mtu; hivyo ni yeye anajua nani akae wapi na nani afanye nini na sio kushinikizwa na watu.