CUF yafukuza wanachama wanane

KIKAO cha Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) katika kikao chake kilichofanyika Vuga Unguja kimepitisha azimio la kuwafukuza uanachama wanane wa chama hicho, wakiwemo watatu ambao walipata kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kipindi kirefu.

Akisoma taarifa za kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 43 kati ya 53, kimekubaliana na maamuzi yaliyotolewa na matawi ya wanachama hao ya kuwafukuza uanachama.

Aliwataja waliofukuzwa ambao walipata kuwa wabunge wa muda mrefu katika CUF kuwa ni Mohamed Habib Mnyaa aliyekuwa Mbunge wa Mkanyageni, Mussa Ali Kombo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake Chake na Khalifa Suleiman Khalifa wa Gando.

Akifafanua, Mtatiro alisema viongozi hao wamefukuzwa uanachama kupitia katika majimbo ya uchaguzi na kuridhiwa na kikao ch Baraza Kuu la CUF kwa madai ya kufanya uasi ndani ya chama zaidi baada ya kuangushwa katika kura za maoni za kuwania ubunge.

“Baraza Kuu la CUF limeridhia kufukuzwa kwa viongozi hao kwa sababu wamekuwa wakifanya vitendo vya kukisaliti chama zaidi baada ya kuangushwa katika kura za maoni za kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Mtatiro.

Aidha, Mtatiro alisema wamempitisha mgombea wa chama hicho katika nafasi ya Bunge la Afrika Mashariki, Twaha Taslima ambaye anaomba nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

Akifafanua, alisema uteuzi wa nafasi hiyo unafanywa na Baraza Kuu ambalo limekaa katika kikao chake na kumuidhinisha kwa kumpa baraka zote kugombea nafasi hiyo na fomu yake kutiwa saini ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Twaha Taslima ni mgombea sahihi wa nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kupitia Chama cha Wananchi na fomu yake imepata baraka za Katibu Mkuu wa CUF kwa mujibu wa masharti yake,” alieleza Mtatiro.