Wakristo wataka ukatili ukomeshwe

UMOJA wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma umewataka Watanzania kuunganisha nguvu za pamoja za kiroho na kimwili na serikali ili kuweza kukomesha vitendo vya kikatili vinavyotokea.

Pia umoja huo umelaani na kukemea vitendo vilivyotokea hivi karibuni vya mauaji ya askari wa jeshi la polisi wapatao wanane na kuwaomba Watanzania kuungana na serikali ili wale wote waliohusika waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kauli hiyo ya umoja huo ilitolewa na Askofu Damas Mukasa wakati akizungumza na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Dodoma mjini.

Aliwataka Watanzania kuungana kwa pamoja na serikali katika kufichua maovu yanayojitokeza kwenye maeneo mbalimbali kama vile ya mauaji ambayo hivi karibuni Taifa limewapoteza askari wake ambao wameuawa na majambazi katika eneo la Kibiti Mkoa wa Pwani.

Alisema serikali pekee haiwezi kufanikisha kuwabaini wanaofanya vitendo ambavyo ni kinyume na katiba ya nchi bali ni pale Watanzania watakapoungana katika kufichua wanaofanya vitendo viovu.

Askofu wa Dayosisi ya Kati Kanisa la Anglikana, Dk Dickson Chilongani ameutaka umoja wa madhehebu mkoani kuhakikisha wanawaunganisha waumini wao na kuwa kitu kimoja ili matatizo yanayojitokeza yaweze kutatuliwa kwa pamoja.

Alisema kama wataungana kwa pamoja bila kujali dini zao, wataweza kuisaidia serikali katika kutatua matatizo yaliyopo kama matukio ya mauaji, ubakaji na utekaji kwa kuzipata taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu wanaoichafua amani iliyopo nchini.

Naye Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dodoma, amewata wananchi wa Mkoa wa Dodoma kuwa tayari katika kupokea fursa zitakazoletwa katika kipindi hiki serikali inahamia.