Sherehe za Muungano kufanyika Dodoma

MAONESHO ya ukakamavu na mbinu za medani katika kupambana na adui katika kulinda amani ya nchi kutoka Kikosi Maalumu cha Makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), itakuwa ni sehemu ya shamrashamra zitakazopamba maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma, Aprili 26 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuhudhuriwa na Rais John Magufuli, pia yatapambwa na burudani nyingine kutoka vikundi mbalimbali.

Mhagama katika taarifa yake alitaja shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika siku hiyo ya Muungano kuwa ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama (JWTZ, JKT, Polisi na Magereza) na onesho la mbwa na farasi waliofunzwa.

Aidha, alisema kuwa mambo mengine yatakayofanyika ni gwaride la uzalendo la wanafunzi wa shule za sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka Dodoma na Zanzibar, bendi ya Yamoto, vikundi vya muziki wa kizazi kipya kutoka kwa wasanii Mchungaji Zayumba, Jacob Beats, Mwenge Jazz na Mgosi Matarumbeta.

“Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na Kuuimarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,” alifafanua Mhagama.

Alitoa mwito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo muhimu kwa kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya nchi. “Ninaomba kuchukua nafasi ya pekee kuwaomba wananchi wote waliopo Dodoma kujitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri siku hiyo ya Aprili 26 mwaka huu, kuanzia saa 12:00 asubuhi ili kusherehekea kwa pamoja maadhimisho hayo muhimu kwa nchi yetu,” alisema.

Maadhimisho ya Muungano yanafanyika kwa mara ya kwanza Dodoma ikiwa ni siku kadhaa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze kutimiza azma ya kuhamia katika makao makuu hayo mapya.