Mawaziri SADC kutathmini siasa Congo

UJUMBE wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara-SADC Troika umewasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) kuanza Misheni ya Pili ya kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini humo.

Ujumbe huo unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, na Mwenyekiti wa SADC wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi naUsalama.

Mawaziri hao ni kutoka Tanzania, Angola na Msumbiji. Misheni hiyo inafanyika baada ya azimio la mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Troika Mbili uliofanyika Swaziland Machi 17 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa juzi ilieleza kuwa, mkutano huo uliagiza kufanyika kwa misheni ya pili ili kuendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hali ya siasa DRC wakati ikifanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Katika Misheni hii yaPili, ujumbe wa Angola utaongozwa na Naibu Waziri wa Mambo yaNje, Manuel Augusto na ujumbe wa Msumbiji utaongozwa na Nyeleti Mondlane, NaibuWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Misheni inatarajiwa kukamilika leo.