Mifuko ya uwezeshaji kiuchumi yaonywa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, kujenga nidhamu katika kutoa huduma zake za mikopo na vitendea kazi kwa wananchi, ili iweze kufikia ndoto zao katika shughuli za kuzalisha mali na taifa liweze kufikia malengo yake ya kiuchumi.

Majaliwa aliyasema hayo wakati akifungua maonesho ya kwanza ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika katika Viwanja vya Mashujaa, Dodoma yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa ajili ya kutoa elimu ya huduma zitolewazo na mifuko hiyo.

“Katika maonesho haya ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na ambayo tunafanya kwa mara ya kwanza, nahitaji kuona kunakuwa na nidhamu ya juu katika utendaji kazi wa kila siku, toeni huduma zenu za mikopo na vitendea kazi bila ya mazingira ya rushwa,” alisema.

Alifafanua kuwa baraza hilo linafanya kazi chini ya Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ndiyo maana limeandaa maonesho hayo, na kuhamasisha mifuko hiyo itambue kuwa imepewa dhamana kubwa kwa taifa ya kuwahudumia wananchi kwa weledi kupata mikopo na vitendea kazi, ili mradi wawe wamekidhi vigezo lakini na kwa masharti nafuu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Being’i Issa alisema serikali ina mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi 19 ambayo kwa ujumla wake ina mitaji ya Sh trilioni tatu na imewafikia wananchi milioni moja.

“Mifuko inafanya kazi ya kuwezesha wananchi kupata mikopo na vitendea kazi na kwenda kuitumia katika katika kilimo, ufugaji, usindikaji mazao na kazi zote za uzalishaji, maonesho haya ni moja ya njia ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za mifuko,” aliongeza.

Alisema pamoja na kufanya kazi hiyo ya kuwezesha wajasiriamali mikopo yenye masharti nafuu lakini bado mifuko hiyo haifahamiki kwa wananchi. Alisema kati ya mifuko 19 iliyopo, ni 13 tu ndiyo iliweza kushiriki maonesho hayo pamoja na wajasiriamali walionufaika na mifuko hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema halmashauri za mkoa wake kuanzia sasa zinahitajika kuongeza kasi katika kushirikiana na mifuko hiyo ili wananchi waweze kuwa na taarifa sahihi za huduma za mifuko hiyo. Maonesho haya yanatarajia kufikia kilele kesho, yameandaliwa na NEEC kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma za mifuko hiyo kwa wananchi.

Kati ya mifuko iliyoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mfuko wa Kuadhamini Wajasiriamali wadogo na wa kati.