‘Mawaziri hawafanyi kazi kwa kuogopa utawala uliopo’

MAWAZIRI hawafanyi kazi kwa kuogopa utawala uliopo bali hufanya kazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, Imeelezwa. Kauli hiyo aliitoa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula (pichani) bungeni jana wakati akitoa taarifa kumweleza Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) aliyesema mawaziri wanafanya kazi kwa hofu.

Naibu Waziri Mabula alisema, hakuna waziri wala naibu waziri anayefanya kazi kwa kuogopa, bali wanafanya kazi kwa kufuata taratibu zilizopo. Msigwa wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi naUtawala Bora) alisema, wajibu wa wabunge ni kuikosoa serikali na serikali inatakiwa kuwajibika kwao, lakini wakiwa bungeni wamekuwa wakizuiwa kuikosoa, kitendo ambacho hakiisaidii serikali.

Msigwa alisema mawaziri wamekuwa waoga na wanafanya kazi kwa woga na hata wamekuwa wakiwakatalia wapinzani kuikosoa na kuipinga serikali, hata kukatazwa kujadili jambo lolote la kuikosoa serikali ya awamu ya tano iliyopo madarakani.

Msigwa alitoa mifano ya viongozi wa serikali mbalimbali duniani na kanisa, kwamba serikali inatakiwa ikubali kukosolewa ili kujipanga vizuri na kuona wapi haifanyi vizuri ili ifanye vizuri kwa kujikosoa.