Walimu kulipwa madeni yao baada ya kuhakikiwa

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi itaendelea kulipa madeni ya walimu wote nchini baada ya kuhakikiwa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) aliyetaka kupata uhakika wa lini madeni hayo ya walimu yatalipwa wakiwamo wa Kaliua.

Stella alisema, serikali itaendelea kulipa madeni hayo kadiri yanavyohakikiwa kutokana na baadhi ya madeni kutokuwa ya uhakika. Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM), aliyetaka kujua serikali italipa lini madeni ya fedha za likizo za walimu, Naibu Waziri Stella alisema, serikali itaendelea kulipa madeni ya walimu pamoja na fedha za likizo.

Manyanya alisema katika kipindi cha mwaka 2015/16, hadi Juni mwaka jana, Sh bilioni 22.6 zililipwa kwa walimu 63,814. Alisema, katika malipo hayo, Sh milioni 13.4 zimelipwa kwa ajili ya madeni ya fedha za likizo kwa watumishi sia wa chuo cha Ualimu Korogwe.

Kuhusu kukapandisha walimu madaraja, Naibu Waziri Manyanya alisema, serikali imekuwa ikipandisha madaraja walimu wanaostahili, katika mwaka wa fedha wa 2015/16, wizara ilipandisha vyeo watumishi 2,272 kati ya hao watumishi 71 ni wa Chuo cha Ualimu Korogwe