RC ataka watu wa madini kutafiti chokaa

MKUU wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa ameagiza ofisi ya Nishati na Madini, Mkoa wa Mara, kuhakikisha inafanya utafiti ili kujua wingi na ubora wa madini ya chokaa na jasi yaliyopo katika kijiji cha kiwasi, Guta na Bulamba wilaya ya Bunda ili mkoa huo uweze kukaribisha wawekezaji.

Dk Mlingwa aliyasema hayo, wakati wa ziara ya kukagua maeneo yaliyo na madini katika wilayani Bunda. Aidha katika ziara yake alitoa Mwito kwa uongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha inamaliza tatizo la uchimbaji wa madini ya chokaa usio rasmi unaofanywa kijiji cha Guta ‘A’ hadi maeneo ya hifadhi ya barabara.

Alisema mkoa huo una rasilimali nyingi na za kutosha na kwamba kutokana na sera ya Serikali ya ujenzi wa viwanda, kuwepo kwa madini hayo kutawezesha mkoa huo kuwa na kiwanda cha kutengeneza saruji na mifuko yake ili vijana wengi waweze kupata ajira.

Aidha, aliwataka wawekezaji kuachana na tabia ya kuchukua leseni za tegesha na badala yake kutumia leseni hizo ili kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi. Ofisa Madini Msaidizi, Samweli Mayuki alisema kuwa ofisi ya madini imekuwa ikifanya utafiti kuwasaidia wananchi kubainisha maeneo ya madini ya viwandani yaliyoonekana katika kijiji cha Kiwasi aina ya jasi .

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Lydia Bupilipili alisema wanaanza mchakato wa kurasimisha kazi hiyo ambapo pia aliwataka viongozi wote kushirikiana kwa pamoja na kuyatatua.

Naye Mkurugenzi wa mji wa Bunda, Janeth Mayanja alisema kuwa walishatoa maelekezo kwa serikali kwa viongozi wa serikali ya vijiji cha Guta ‘A’ ili waweze kuwapatia leseni na kwamba asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa na wanakijiji hao yatabaki kwao huku asilimia 80 ikibaki katika uongozi wa halmashauri ya mji huo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Noah Okumu alisema mradi wa uchimbaji huo ulianza kijijini hapo mwaka 2007 ambapo ulikuwa mradi wa wanakijiji na kwamba wakishachimba chokaa inauzwa kwa kiasi cha Sh 2,500 kwa mfuko mmoja wa chumvi chumvi ambapo wanapata kiasi cha Sh milioni 1 kwa mwaka.