Samia aiagiza TRA kutatua kero za wafanyabiashara

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere ahakikishe anaweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara kwa mara kama njia ya kujadili na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hao.

Makamu wa Rais alisema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Kichere kuhusu namna bora ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara nchini kama hatua ya kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi wa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Alisema anasikitishwa na baadhi ya maofisa wa TRA kuwanyanyasa wafanyabiashara na wengine kuwabambikizia kodi kubwa, hali ambayo inazua malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kama TRA itafanya mabadiliko yoyote ya ulipaji wa kodi ikawafahamisha wafanyabiashara hao mapema ili kuondoa usumbufu mkubwa unaoweza kutokea katika ulipaji wa kodi pindi wanapoagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Makamu wa Rais alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha ulipaji wa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa unafanyika kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu na sio kuwakandamiza Watanzania kwa kuwalipiza kodi mara mbili, jambo ambalo alisema halifai hata kidogo.

Makamu wa Rais alimtaka Kamishna wa TRA kukomesha mara moja tabia ya baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo kutoa lugha chafu na kuudhi kwa wafanyabiashara bali watumie lugha nzuri ili kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari bila kulazimishwa na mtu.

Hata hivyo, aliipongeza TRA kwa kazi kubwa inayoifanya katika ukusanyaji wa mapato na amewapa moyo wa kuongeza bidii katika ukusanyaji wa kodi hizo ambazo Serikali inatumia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Kichere alimuahidi Makamu wa Rais kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha malalamiko mbalimbali yanayotolewa na wafanyabiashara yanapata ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Kamishna Kichere amesisitiza kuwa kwa baadhi ya maafisa wa Mamlaka hiyo wanaokiuka maadili ya kazi ataendelea kuwachukulia hatua stahiki ili kurejesha nidhamu katika utendaji wa kazi na ukusanyaji wa mapato