Ngome za Chadema kuvunjwa

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) tawi la Sokola Kata ya Majengo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, umejipanga vyema kuvunja ngome za wapinzani wao Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) katika vijiwe vya kahawa vilivyopo katika maeneo yao.

Umoja huo umesema kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu katika kipindi cha mwaka 2015 na kuwapata viongozi mbalimbali ngazi ya udiwani, ubunge na urais, kumekuwepo na minong’ono isiyokuwa na tija katika vijiwe vya kahawa kwamba viongozi tawi hilo la sokola hawafanyi lolote.

Waliyasema hayo juzi katika kikao chao cha ndani kilichoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho Kata ya Majengo, Noel Museveni ambapo walipanga mikakati hiyo ya kuvunja ngome hiyo ili wafanye shughuli badala ya kukaa na kuwasema vibaya viongozi walioko madarakani.

Aidha Museveni aliwataka vijana wote katika umoja wao kushikamana kwa pamoja ili kukomesha hali kama hiyo kwani wanachama wa Chadema wanapaswa kufanya kazi na si kukaa vijiweni.

“Kama mmebaini hiyo hali na ili mkamilishe lengo, vijana wote katika umoja wenu unganeni na kufanya kazi kama timu ya kuvunja ngome hiyo, na kazi ya kuvunja ngome si kuleta vurugu, ninyi mnapaswa kujiunga na hiyo ngome na kuanza kuwashawishi masuala ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwashauri kufanya kazi kwani majungu hayasaidii,” alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Majengo, Benard Mahongo aliyehudhuria kikao hicho, alisema kuwa yeye binafsi amekwishaanza kukabiliana nao kwa kuwapa kazi ndogo ndogo na tayari wapo waliomhakikishia kurudisha kadi za Chadema katika kipindi kijacho cha uchaguzi mkuu 2020.