Mwisho wa Shisha Julai 4, sasa sheria kutungwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ina mpango wa kutunga sheria itakayodhibiti na kupiga marufuku utumiaji, uuzaji na usafirishaji wa shisha nchini.

Waziri huyo amebainisha kuwa kwa sasa mikoa kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha imeanza kupiga marufuku matumizi, uuzaji na usafirishaji wa shisha ikiwa ni mkakati wa kuokoa afya za wananchi wanaoathriwa nayo. Aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalum, Najma Giga (CCM) aliyetaka kujua kama serikali inaendelea kuruhusu matumizi ya Shisha kwenye baadhi ya migahawa na hoteli kubwa nchini ambayo inatumiwa na watu wa rika zote.

Alisema utumiaji Shisha umebainika kuwa ni kati ya aina ya uvutaji wa sigara ambao wauzaji wengine huchanganya na aina mbalimbali za dawa za kulevya na vileo vikali na kusababisha vijana wadogo kuathiriwa nayo kwa kiasi kikubwa. Nchemba alisema, baada ya serikali kuona matumizi ya Shisha yanaathiri afya ya binadamu kutokana na utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, baadhi ya maeneo nchini yaliipiga marufuku.

Hata hivyo, alisema wakati sheria hiyo ikisubiriwa kutungwa, tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku matumizi ya Shisha ifikapo Julai 4, mwaka huu. Akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyehoji wafanyabiashara wenye leseni za kuuza na kusafirisha Shisha watafanyaje, Nchemba alisema kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuokoa maisha ya Watanzania wasiathirike. “Masuala yanayohusu afya za Watanzania ndio kipaumbele cha serikali.

Jambo la kwanza ni kuokoa maisha ya watu ndio maana tunaandaa utaratibu wa kushughulikia suala hili kisheria,” alifafanua. Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alitaka kujua mkakati wa serikali kuokoa vijana waliokata tamaa kutokana na ugumu wa maisha hali iliyochangia wajiingize kwenye utumiaji shisha, dawa za kulevya na bangi. “Tangu serikali ipige marufuku matumizi ya viroba kutokana na ugumu wa maisha vijana sasa wameanzisha kilevi kingine, wanatumia gundi,” alisema.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kwa sasa serikali inatumia mkakati wa kutoa elimu kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku na pombe. “Lakini pia tumeanzisha mpango wa kupanua huduma za vituo vinavyotoa tiba ya waathirika wa dawa za kulevya.

Tutaanzisha vituo hivyo Tanga, Arusha, Mbeya na maeneo mengine. Ila tunaomba wazazi nao watimize wajibu wao,” alisisitiza. Naye Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu ambaye pia ni mbunge wa Ilala (CCM), aliwataka wabunge wasiliache suala hilo mikononi mwa serikali pekee kwani matumizi ya dawa za kulevya, shisha na pombe kwa vijana ni mzigo wa jamii nzima wakiwemo wazazi husika.