Serikali yaagiza DMO kudhibiti fedha za vifaa tiba, dawa

SERIKALI imewataka waganga wakuu wa wilaya (DMO) kuhakikisha fedha zote zinazotengwa kununulia dawa na vifaa tiba katika halmashauri nchini, zinatumika ipasavyo ili kutowabebesha wananchi, mzigo wa kununua vitu hivyo.

Agizo hilo limetolewa bungeni Dodoma jana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo baada ya baadhi ya wabunge kulalamika bungeni hapo kuwa, katika halmashauri nyingi kuna ukosefu wa dawa na vifaa tiba ambapo wajawazito na watoto, hulazimishwa kujinunulia. Jafo alikuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama (CCM) na Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda.

Katika swali lake la nyongeza, Gama, alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za akina mama na watoto katika hospitali ya rufaa ya Ruvuma kwa kuwa wawapo hapo, hulazimika kununua dawa na kutakiwa kuja na vifaa vya kujifungulia ikiwemo damu na mipira ya kuvaa mkononi. Naye Mapunda alibainisha kuwa matatizo yanayoikumba hospitali ya rufaa ya Ruvuma ni sawa na yanayoikumba hospitali ya Mbinga ikiwemo hospitali hiyo kuhudumia halmashauri tatu kwa wakati mmoja na hivyo kuelemewa.

Akijibu maswali hayo, Jafo, alisema ameyapokea malalamiko ya wabunge hao na kubainisha kuwa akina mama na watoto hawapaswi kununua dawa na vifaa tiba kwa kuwa serikali hupeleka fedha katika kila halmashauri kwa ajili ya kazi hiyo. “Lakini naona bado kuna tatizo watu hawapati dawa wala vifaa tiba. Nawaelekeza ma DMO wote nchini kuhakikisha fedha zinazotumwa kwao kwa ajili ya dawa na vifaa tiba zinatumika kama inavyotakiwa,” alisisitiza Jafo. Alisema hata Rais John Magufuli alishatoa fedha kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba katika kila halmashauri hivyo endapo haziwafikii wananchi, ni changamoto atakayoifanyia kazi.