Mwigulu aagiza IGP kufuatilia tukio la Malima

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Inspekta Jenerali Ernest Mangu, achunguze tukio la askari polisi anayedaiwa kufyatua hovyo risasi na kumtisha kwa risasi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha Adam Malima.

Mwigulu aliyasema hayo katika viwanja vya Bunge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumtaka atoe kauli kuhusu tukio hilo. Alisema kwa sasa hawezi kutoa tamko lolote hadi pale atakapopata taarifa kamili kwa pande zote kuhusu nini hasa kilichotokea hadi kuibuka kwa hali hiyo ya kufyatuliana risasi.

Hata hivyo, waziri huyo, alikiri kuwa tayari ameiona video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayomuonyesha askari huyo katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam akifyatua risasi hewani na kumtishia Malima kwa bunduki.

Awali, ndani ya Bunge mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu akitaka kujua ni hatua gani zitachuliwa na Serikali ili kukabiliana na matumizi ya silaha hadharani.

Mbunge huyo alifafanua kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya aina yaliyotokea hivi karibuni akitoa mfano tukio la kituo cha Clouds na baadaye mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliyetishiwa pia kwa bastola na askari.

Katika hatua nyingine, Adam Malima ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, na dereva wake, Ramadhani Kigwande wamefikishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kujeruhi na kumzuia Askari Polisi H 7818 PC Abdu, kufanya kazi yake.

Malima ambaye alikuwa Mbunge wa Mkuranga na dereva wake, walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Respicious Mwijage. Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai katika mashitaka ya kwanza kuwa, tukio hilo lilitokea Mei 15 mwaka huu, maeneo ya Masaki Kinondoni.

Alidai Kigwande kwa nia ya kukataa kukamatwa kutokana na kuegesha vibaya gari lake lenye namba za usajili T 587 DDL, alimjeruhi Mwita Joseph ambaye ni Ofisa Operesheni kutoka Kampuni ya Priscane Business Enterprises na kusababishia maumivu makali.

Katika mashitaka ya pili, Kombakono alidai Malima alitenda kosa la shambulio, tukio lililotokea Mei 15 mwaka huu maeneo ya Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam. Alidai Malima alimzuia Askari Polisi mwenye namba H 7818 PC Abdu kufanya kazi yake halali ambaye alikuwa anamkamata Kigwande aliyefanya makosa ya kumshambilia Joseph.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana. Wakili wa washitakiwa, Peter Kibatala aliiomba mahakama hiyo kutoa masharti nafuu ya dhamana kutokana na asili ya mashitaka hayo. Pia alidai Malima ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, ni mtu anayetambulika katika jamii kwa kuwa alikuwa Mbunge na Naibu Waziri.