Madereva watakiwa kutimiza wajibu wao

MADEREVA nchini wametakiwa kutambua kuwa wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua huku wakitambua kuwa barabara ni mali ya umma kwa kuendesha vyombo vya moto kwa kujihami.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani, Henry Bantu Mkoani hapa ambapo alisema kuwa madereva wana wajibu mkubwa wa kuchangia katika kuhakikisha wanalinda usalama barabarani.

Aliwataka madereva kuwa makini na hatari zinazotegemewa kwa kuendesha vyombo hivyo huku wakiwa wanajihami na hatari hizo. Bantu alisema kuwa dereva wa kujiahami lazima ajue kuwa barabarani kuna hatari, na kwamba hatari zote sio hatari kuna hatari zilizopo na hatari za kutegemewa.

Aidha, aliwataka madereva hao kuacha tabia ya kuoneana wao kwa wao ambapo alisema kuwa kumekuwa na tabia ya madereva wa magari makubwa kuwaonea wa magari ya madogo huku nayo yakizionea pikipiki na baadaye nao kumuonea anayetembea kwa miguu.