Majaliwa kutoa maelekezo mgawanyo wafanyakazi CD

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuitisha kikao cha watendaji wanaohusika kugawanya wafanyakazi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenda katika maeneo mapya ya kazi, ili kuwapa maelekezo ya namna ya kushughulikia suala hilo.

Hatua hiyo inatokana na agizo la Rais John Magufuli la Jumatatu ya Mei 15, mwaka huu alipokuwa akiivunja mamlaka hiyo kwamba wafanyakazi wote wahamishiwe katika maeneo mengine ya kazi, ikiwemo Halmashauri ya Manispaa Dodoma.

Aidha, alisema kuwa atampangia kazi nyingine aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Paskasi Muragili. Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kufanikisha mgawanyo wa wafanyakazi 265 wa CDA kwenda kwenye maeneo mapya ya ajira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema wanamta rajia Waziri Mkuu kuitisha kikao wakati wowote kati ya jana au leo ili kuwapa maelekezo ya jinsi ya kushughulika na suala hilo.

Kwa mujibu wa Simbachawene, suala hilo haliwezi kufanyika kiholela, hivyo ni lazima wasubiri maelekezo na miongozo kutoka kwa Waziri Mkuu, ili walitekeleze kwa namna nzuri inayostahili.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ndio inayoratibu suala hilo la kuwagawanya wafanyakazi wa CDA kwenda kwenye maeneo mengine ya kazi, hivyo hatuna budi kusubiri kupewa maelekezo kuhusu kila linalotakiwa kufanyika, hatua kwa hatua.”

Rais pia aliivunja Bodi ya CDA, iliyokuwa ikiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenister Mhagama.

Wakati akiivunja mamlaka hiyo iliyoanzishwa kwa Amri ya Rais, Aprili 1, 1973, na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230, aliagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi.