Waziri akemea kauli za kuchochea chuki bungeni

MSEMAJI wa Kambi ya Upinzani bungeni kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mwita Waitara amejikuta katika wakati mgumu, baada ya kubanwa na Serikali na kulazimika kufuta maeneo yote yenye utata yaliyopo kwenye hotuba yake aliyoiwasilisha bungeni, baada ya kushindwa kuthibitisha kuwa yana ukweli.

Waitara alikumbwa na kadhia hiyo, bungeni mjini Dodoma juzi wakati wa mjadala wa kupitishwa kwa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo ya ulinzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.

Hoja za kumtaka kiongozi huyo wa upinzani afute kauli zake zinazodaiwa kuwa za uongo au azithibitishe, zilitolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Husein Mwinyi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu na Bunge Jenista Mhagama na baadaye kusisitizwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan Zungu.

Awali kabla ya kuibuliwa kwa hoja hiyo, Dk Mwinyi wakati akihitimisha hoja ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, aliyaainisha maeneo yote yenye utata yakiwemo yaliyofutwa mapema kabla ya kusomwa kwa hotuba hiyo na Spika wa Bunge, Job Ndugai, na kusisitiza kuwa ni ya uongo na aliyewasilisha hotuba hiyo bungeni anapaswa kuyathibitisha.

Alisema zipo rejea za Katiba, amri za mkuu wa majeshi na sheria za nchi zinatoa utaratibu wa namna ya jeshi hilo linavyotakiwa kufanya kazi pamoja na namna wanajeshi wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao.

Alisema hotuba hiyo ya upinzani inaingilia mno majukumu ya jeshi, kwani imechukua maneno kutoka kwa askari wasiozingatia nidhamu, bila kufanya utafiti wa kutosha na kugeuza maneno hayo kuwa ndio kauli ya kambi hiyo.

“Kauli kama hizi zinasababisha kupandikiza mbegu za utovu wa nidhamu jeshini,” Akizungumzia madai ya kambi hiyo ya upinzani kuhusu bodi ya manunuzi ya wizara hiyo kujipa dhamana ya manunuzi nje ya nchi, alisema bodi inawajibu wa kutoa idhini ya manunuzi lakini wajumbe wa bodi hiyo hawana wajibu wa kufanya manunuzi.

Kwa upande wake, Zungu alikiri kuwa tangu awali kabla ya kusomwa kwa hotuba hiyo alitahadharisha kutokana na ukweli kuwa sheria na kanuni za Bunge hilo haziruhusu wabunge kusema uongo na endapo itatokea hali kama hiyo, mhusika ama atatakiwa athibishe au afute maneno hayo ya uongo.

Waitara aliposimama alibainisha kuwa mengi ya masuala yaliyoibuliwa tayari yalishafutwa na Spika Job Ndugai na miongozo ya mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika ambayo ilibainisha kuwa maeneo hayo yanakiuka Kanuni za Bunge.

Hata hivyo, baada ya kubanwa na kutakiwa afute tu maeneo hayo yenye utata kwenye hotuba yake ili yasiingizwe kwenye kumbukumbu za Bunge au athibitishe, Waitara alitamka kuwa ameyafuta maeneo hayo na maneno ya Dk Mwinyi ndio yachukuliwe kuwa ya ukweli.