Waandishi wakamatwa na Polisi Arusha, waachiwa

WAANDISHI wa vyombo mbalimbali vya habari mkoani Arusha akiwemo Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali.

Wengine waliokamatwa jana ni pamoja na madiwani wawili na viongozi wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) na baadhi ya viongozi wa dini. Hata hivyo, baada ya kufikishwa Polisi, waandishi waliachiwa kwa maelezo kuwa, walikamatwa kimakosa.

Kusanyiko hilo lilielezwa lilikuwa na lengo la kuwapa rambirambi wazazi waliofiwa na watoto katika ajali ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vicent ya jijini hapa. Ajali hiyo ilitokea eneo la Rhotia, Karatu wakiwa katika safari ya kimasomo Mei 6 mwaka huu na kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

Waandishi hao baadhi walikamatwa na polisi shuleni hapo pamoja na viongozi waliombatana nao kisha kupakizwa kwenye magari ya polisi hadi kituo kikuu cha Polisi kilichopo Mjini Kati jijini hapa.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo alisema mmoja kati ya viongozi wa Tamongsco, Kanda ya Kaskazini alikuwa na Sh milioni 18 kwa ajili ya kutoa rambirambi kwa wafiwa lakini ilishindikana baada ya kukamatwa na polisi waliofika shuleni hapo.

Miongoni mwa waandishi waliokamatwa ni pamoja na Godfrey Thomas (Ayo Tv), Alphonce Kusaga (Triple A), Hussein Tuta (ITV), Joseph Ngilisho (Sunrise Radio), Filbert Rweimamu (Mwananchi), Janeth Mushi (Mtanzania), Elihuruma Yohani (Tanzania Daima) na Idd Uwesu (Azam Tv) Madiwani waliokamatwa na kuachiwa ni pamoja na wa kata ya Olasiti, Alex Marti na wa kata ya Muriet, Credo Kifukwe ambao walikuwa pamoja na timu ya viongozi wa dini na wa Tamongsco pamoja na viongozi wa dini baadhi ambao hawajajulikana majina yao.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ilembu, waandishi hao walikamatwa kimakosa hivyo waliachiwa huru