Wahimizwa kutumia mboga kupunguza utapiamlo

WATOTO chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wenye umri wa miaka 14 hadi 35 waliogundulika kuwa na utapiamlo mkali uliotokana na ukosefu wa viini lishe vinavyopatikana kwenye mboga, wamehimizwa kutumia mboga zenye virutubisho na jinsi ya upikaji bila kuathiri virutubisho ili kupunguza utapiamlo.

Shirika lisilo la kiserikali la World Vegetable Center linalodhaminiwa na Shirika la Misaad la Marekani(USAID) lilitoa mafunzo hayo ya kilimo cha mboga kilichohusisha vijiji 18 vya Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara na kukabidhi baiskeli 18 kwa wakufunzi wa kilimo cha mboga ngazi ya kijiji wilayani Babati mkoani humo, baada ya kufanya utafiti na kugundulika kuwa na tatizo la utapiamlo kwa baadhi ya watoto unasababishwa na ukosefu wa viini lishe vinavyopatikana kwenye mboga.

Akizungumza na wakufunzi hao kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini, Ofisa Mipango wa halmashauri hiyo, Denitho Kavenuke alisema lengo kuu la mradi huo ni kupunguza utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano na wanawake wenye umri wa miaka 14 hadi 35.

Mafunzo yaliyotolewa kwa wakufunzi hao ni ya utaarishaji wa bustani aina ya vichuguu, viroba na matuta pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya mboga zenye virutubisho na jinsi ya upikaji bila kuathiri virutubisho.

Mradi uliweka mpango wa kuwawezesha wakulima wakufunzi hao kuwapatia usafiri wa baiskeli ili waweze kuwafikia wakulima wengi zaidi walio kwenye vikundi vyao ili kuwapa elimu hiyo ya kilimo cha mboga.