Wakandarasi waliovurunda kunyimwa zabuni za ujenzi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, imepiga marufuku wakandarasi waliobainika kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara chini ya kiwango kutopewa tena zabuni za ujenzi huo na kuamriwa kuwa iwe ni mara ya mwisho barabara kujengwa chini ya kiwango.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Frank Tarimo alisema hayo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani ambacho kilijadili miradi mbalimbali ya maendeleo. Alisema halmashauri haiwezi kuruhusu fedha za wananchi zikaendelea kupotea wakati baadhi ya wakandarasi wakitumia vibaya fursa wanazopewa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miradi ya barabara kuwa chini ya kiwango.

Aidha mwenyekiti huyo alitaka halmashauri ya wilaya kumuwezesha mhandisi wa ujenzi fungu maalum la fedha kwa ajili ya kutembelea miundombinu mbalimbali hususan barabara kwani kinyume na hapo ni kutothamini utaalamu wake.

Awali diwani wa kata ya Kirua, Robert Mrisho alitaja baadhi ya barabara ambazo zinazodaiwa kujengwa chini ya kiwango na kutaka halmashauri kuchukua hatua kwa wakandarasi waliohusika.

Alitaja barabara hizo kuwa ni Mwl Anaely/Kengia iliyogharimu zaidi ya Sh milioni 118.3 na Sanya juu/Naibili/Kia, ambazo kwa pamoja licha ya kutumia mamilioni ya fedha zimeharibika katika kipindi kifupi baada ya kutengenezwa jambo linaloashiria matumizi mabaya ya fedha za umma. Katika majibu yake ya msingi, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Monica Sana alisema tayari mipango imeandaliwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora.