Wafanyakazi wa muda mrefu vituoni sasa kuhamishwa

WAFANYAKAZI waliokaa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi watahamishwa ili kwenda kutoa huduma mahali pengine kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi kazini. Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Mwanjelwa (CCM) alihoji mkakati wa serikali kuhusu kuwahamisha wafanyakazi waliofanya kazi kwa muda mrefu na wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Suleiman Jafo alisema wafanyakazi ambao walifanya kazi katika vituo kwa miaka 15 au 20, watatakiwa kuhamishwa ili kwenda mahali pengine kwa ajili ya kuleta ufanisi zaidi.

Katika suala la msingi Mary Mwanjelwa aliuliza mkakati na sera ya serikali kwa wafanyakazi hususan walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara.

Jafo alisema kanuni za huduma za utumishi wa umma za mwaka 2009, watumishi wa umma hupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa na ufanisi katika utendaji kazi. Alisema mwalimu anapohitimu mafunzo yake anastahili kubadilishwa muundo wake wa utumishi mfano mwalimu wa daraja III stashahada kwenda daraja la II ngazi ya shahada.

Jafo alisema kupanda kwa madaraja kwa watumishi kunategemea utendaji kazi unaothibishwa na matokeo katika mfumo wa wazi wa upimaji utendaji kazi wa utumishi husoka (OPRAS). Alisema watumishi wote wanatakiwa kujaza fomu hizo na kupimwa utendaji wao kama wanasthaili kupandishwa madaraja.