Kesi ya Manji yaahirishwa hadi Juni 23

KESI ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji anayemiliki Kampuni ya Quality Group imeahirishwa hadi Juni 23, mwaka huu kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Manji ambaye ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, alifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha. Awali, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mkeha alikubaliana na maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 23 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Manji anashitakiwa kwa mashitaka ya kutumia dawa za kulevya kinyume na kifungu namba 17 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia dawa za kulevya namba tano ya mwaka 2015.

Inadaiwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Februari 6 na 9 mwaka huu, maeneo ya Upanga, Sea View wilayani Ilala mkoa wa Dar es Salaam, ambapo alitumia dawa za kulevya aina ya heroin (diacety -morpline). Hata hivyo, Manji yupo nje kwa dhamana ya Sh milioni 10 aliyosaini pamoja na mdhamini wake.