Samia aagiza hatimiliki ardhi oevu zibatilishwe

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika kwa uhakiki wa hatimiliki zote zilizotolewa kwenye ardhi oevu na kuzibatilisha haraka iwezekanavyo ili kuokoa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu.

Alitoa agizo hilo mjini Dodoma jana wakati wa kupokea Taarifa ya Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuokoa Mifumo wa Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kilichoundwa na Ofisi yake ili kukoa uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu.

Makamu wa Rais pia aliagiza watendaji wa ofisi yake washirikiane na Tamisemi kuhakikisha wanawaondoa watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi ya bonde hilo mara baada ya kumaliza kuvuna mazao yao. Alisema hatua hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kurejesha hali ya uoto wa asili ulioharibiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Samia alisisitiza kuwa sheria zote zinazohusiana na usimamizi endelevu wa ikolojia na mazingira ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu ikiwemo sheria ya mazingira na nyingine zitekelezwe kwa ukamilifu na kila mhusika.

Alisema kuwa ili kutekeleza maagizo hayo ni vyema wadau wote wa mazingira washirikiane kikamilifu na kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika ili wajione nao ni sehemu ya mkakati wa kuokoa mfumo wa ikolojia wa bonde hilo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao na maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema kikosi kazi hicho ambacho kilizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Aprili 11, mwaka huu mjini Iringa kimefanya kazi kubwa kwa siku 30.

Alisema ana uhakika taarifa ya kikosi kazi hicho ikifanyiwa kazi ipasavyo italeta mabadiliko makubwa katika Uhifadhi wa Ikolojia katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu na kurejesha hali yake ya awali.

Waziri Makamba alisema kazi kama hiyo itafanyika katika maeneo mbalimbali nchi ili kuhakikisha uharibifu kwenye mabonde yote nchini inakomeshwa na kwamba jitihada zilizochukuliwa na ofisi yake tayari zimewavutia baadhi ya wahisani ambao tayari wameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali katika Uhifadhi wa mazingira nchini.

Baadhi ya Mawaziri ambao walipewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo waliahidi kutekeleza haraka iwezekanavyo maelekezo ya Makamu wa Rais ili kukomesha uharibifu mkubwa wa mazingira katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu