CAG mstaafu apongeza ‘panga’ vyeti feki

ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoh ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa hatua ya kushughulikia wafanyakazi hewa na wenye vyeti vya kughushi, kwani ushauri wa namna hiyo ulitolewa miaka mingi iliyopita bila mafanikio.

Utoh ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji ya taasisi ya WAJIBU Institute of Public Accountability, alisema jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo wa kuchambua ripoti ya CAG ya 2015/16.

Madhumuni ya kuwepo kwa mkutano huo ni kuwezesha wananchi kuelewa taarifa za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ili kuboresha uwajibikaji na utawala bora. Alisema kucheleweshwa kuchukua hatua kwa utekelezaji huo wav yeti feki na wafanyakazi hewa kumeipotezea serikali mabilioni mengi.

Alisema kikatiba na kisheria CAG ana jukumu kubwa la kuishauri serikali hivyo anapotoa mapendekezo yanakuwa hayatekelezwi. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kijamii (Foundation for Civil Society), Francis Kiwanga alisema kazi yao kubwa ni kusukuma ajenda ya utawala bora na hivi sasa wanafurahia kwa kuwa tayari taarifa muhimu zinaanza kuandaliwa katika lugha rahisi. “Kama taasisi za kijamii tunaungana na kazi yetu kubwa ni kusukuma ajenda ya uwajibikaji,” alisema.