Serikali kuunda kikosi kazi cha matatizo ya wafugaji

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema ataunda kikosi kazi maalumu kuchunguza matatizo yanayowakuta wafugaji nchini ili Serikali iweze kuwasaidia kuyatatua.

Miongoni mwa matatizo hayo ni kukosekana kwa maeneo rasmi, yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo nchini. Samia alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania, ambao walimweleza matatizo na manyanyaso wanayopata wakiwa katika shughuli zao za ufugaji.

Alisema amepokea mapendekezo yao na Serikali itafanyia kazi kuondoa hali ya sintofahamu, inayowakuta wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa sasa. Makamu wa Rais pia aliwataka wafugaji waache kutumika kama mtaji wa kisiasa, kwani kufanya hivyo kutarudisha nyuma jitihada za kuimarisha na kuboresha shughuli zao nchini.

Alisema ili kujua kwa kina hali ilivyo, Serikali itaunda kikosi kazi hicho na kitatembelea maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo yenye migogoro kuhakikisha suluhu ya matatizo hayo, ikiwemo migogoro kati ya wafugaji na wakulima inapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye, akisoma taarifa ya wafugaji hao kwa Makamu wa Rais, alieleza kuwa kukosekana kwa maeneo ya malisho, ndio chanzo kikubwa cha kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi za taifa na wawekezaji nchini.

Alisema kama Serikali za mikoa na wilaya kote nchini, zitaiga mfano wa mikoa ya Katavi na Ruvuma ambayo imeshatenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, migogoro kama hivyo nchini itakuwa ni historia.

Katibu huyo aliiomba Serikali kuwapatia mashamba makubwa, ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji ili nao waweze kufanya shughuli zao za ufugaji katika maeneo hayo. Alieleza kuwa kama Serikali itawapatia maeneo maalum kwa ajili ya kufuga, sekta ya mifugo nchini itawavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao wataanzisha viwanda.