Rais Magufuli, bosi Barrick wapongezwa

WASOMI, wachambuzi wa masuala ya uchumi na wanadiplomasia, wamepongeza hatua ya maridhiano ya kukaa meza ya mazungumzo, iliyooneshwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton aliyefanya mazungumzo juzi na Rais John Magufuli.

Wamesisitiza kuwa hiyo ni nia ya dhati ya kufanya biashara yenye maslahi kwa pande zote. Akizungumza jana kwa nyakati tofauti na HabariLeo jijini Dar e Salaam, Mwanadiplomasia na aliyekuwa Katibu wa Mwalimu Julius Nyerere, Balozi Charles Sanga alisema Rais Magufuli anaona mbali mno na anafanya hayo kwa maslahi ya taifa.

“Nimefanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu, na mara nyingi nilikuwa naye na maono yake ndiyo haya haya anayofanya Rais Magufuli, kuja kwa kiongozi huyo ni moja ya kutambua na kuthamini kazi anazofanya rais,” alisema Balozi Sanga.

Alisema, awali wakati wa kupokea ripoti ya kamati zote mbili, Rais aliweka wazi msimamo wake na wa nchi kuwa anakaribisha meza ya mazungumzo na kwamba hatua za kiongozi huyo kuja ni kutambua uwepo wa nafasi hiyo katika kufikia maridhiano ya faida kwa pande zote.

Balozi Sanga alisisitiza kuwa pamoja na kampuni hiyo, kukubali kukaa meza ya mazungumzo, ni vyema mazungumzo hayo yakafanywa kwa umakini na sio katika hali ya udhaifu, kwani maslahi ya nchi ni lazima yapiganiwe kwa nguvu zote.

“Meza ya mazungumzo katika Diplomasia ni jambo jema, ila lazima lifanywe na umakini na sio kwa udhaifu kwani suala la maslahi ya nchi halina kubebelezana”,alisisitiza Balozi Sanga. Aliongeza kwa upande mwingine hatua ya kuja kwa kiongozi huyo ni kuonesha uhusiano mzuri uliopo baina ya Canada na Tanzania, ambao wamekuwa marafiki wa siku nyingi tangu enzi wa Mwalimu Nyerere.

“Nakumbuka mara ya mwisho tulivyoenda Vancouver, Canada na Mwalimu Nyerere ilikuwa ndio mwanzo wa mazungumzo kuhusu ujenzi wa bomba la gesi ya Songosongo, na katika mazungumzo yake na viongozi wa Canada, walikubaliana kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa faida kwa pande zote, sasa wameona huyo Magufuli ana maono ya Nyerere na wakaamua kuja,” alisema Balozi Sanga.

Hata hivyo, aliwaonya wanasiasa wanaoendeleza mjadala usio na tija kwa maslahi ya taifa na kuwataka wabadilike kifikra na kuunga mkono juhudu zinazofanywa na Rais Magufulli za kusimamia maslahi ya taifa kwanza.

“Kama wanasema taarifa ya tume hizo mbili zina taarifa za kupika, unafikiri hao wazungu ni wajinga kiasi hicho, apoteze fedha kutoka Canada kuja hapa kwa taarifa za uongo? Ifike mahala masuala ya maslahi ya Taifa tuyaunge mkono,” alisisitiza Balozi Sanga.

Alitoa mfano kuwa alipokuwa na Mwalimu Nyerere, alisisitiza siku zote kuwa hakuna muda wa kupoteza linapokuja suala ya maslahi ya taifa; na kusema anashangaa kwanini watu wanashindwa kusema hapana.

“Wanasiasa wa kweli lazima wafike mahali waseme basi, Rais anafanya vizuri na Barrick wamekuwa wajanja na wameona kuliko wapoteze ni heri warejee kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu hivi sasa biashara ni huria inaweza kuchukuliwa na nchi nyingine kama China,” alisema Balozi Sanga.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema meza ya mazungumzo ni hatua mzuri kwenye masuala ya biashara.

DK Bana alisema jambo la msingi ambalo Tanzania inapaswa kufanya ni kuzingatia katika mazungumzo hayo, kunawekwa hadidu za rejea vizuri ili ziwe mwongozo utakaokuwa na maslahi ya taifa.

“Kuja kwa kiongozi huyo ni busara na hii ni hekima ya rais tangu awali aliposema anakaribisha mazungumzo, tunachosisitiza ni kwamba katika mazungumzo hayo tuwatumie wataalamu wetu wazuri akiwemo Waziri wetu wa Katiba na Sheria, Profesa Kabudi, ninamheshimu sana, ili kufikia mwisho mwema,” alisema Dk Bana.

Alisema katika mazungumzo hayo, siyo vibaya kama itabidi kuomba wabobezi wa masuala hayo, kusaidia kwenye ushauri ili mwisho wa siku pande zote zinufaike na kubwa zaidi ni kulinda rasilimali za taifa.

Akizungumzia matumizi ya fedha hizo iwapo kampuni hiyo itazilipa kama ilivyosema, Dk Bana alisema Tanzania ina Mpango wa Maendeleo wa Taifa na hata ule wa Maendeleo wa mwaka 2030, hivyo ni vyema vipaumbele vilivyotaja vikazingatiwa katika matumizi ya fedha hizo.

Akizungumzia kuhusu wanasiasa nchini, Dk Bana alisema masuala ya maslahi ya taifa hayana vyama na sio busara kutafuta umaarufu wa mtu au chama kwenye jambo hilo. “Tunasikia neno laana ya rasilimali za Afrika, na Tanzania tumeonesha mfano kuwa sisi hatumo kwenye hilo kwa kuamua kuchukua hatua ili biashara hiyo iwe ya faida kwa maslahi ya taifa, sasa wanasiasa wanaopinga hili wajue kuwa hili sio la maslahi binafsi au vyama vyao, wasubiri wakati wa kampeni ndiyo wafanye hayo, hapa sio mahali pake,” alisisitiza Dk Bana.

Alishauri wanasiasa wote nchini waungane na kusaidia kupatikana kwa tume bora itakayokuja na muafaka kwenye majadiliano na kusema angefurahi pia iwapo tume hiyo, itawahusisha pia wabunge wenye sifa na faida kwa maslahi ya taifa bila kujali vyama vyao.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Profesa Haji Semboja alisema kuja kwa kiongozi huyo ni jambo la ustaarabu na ni mwanzo mzuri, kwani sio jambo la kwanza kufanyika, na kutoa mfano kuwa hata kwenye suala la Kampuni ya Saruji ya Dangote, mazungumzo kama hayo yalifanywa.

Profesa Semboja alisema hatua zinazofanywa na Rais Magufuli ni za kuinua uchumi wa viwanda na kwa hatua hiyo Tanzania itafanya vizuri kwenye sekta ya uchumi kwa kuweka mipango mizuri ya matumizi ya rasilimali hiyo.

“Kuna faida mbili hapa zinaonekana, kwanza sheria za madini zikishakamilika kufanyiwa mapitio na kuwa bora zitafanya rasilimali hii ilete faida kwenye uchumi wetu, tutajenga viwanda vya kutengeneza vito na mapambo ya madini hayo hapa hapa nchini hivyo kuleta fedha za kigeni.” alisema Profesa Semboja.

Pia alisema madini yanayopatikana nchini, yanaweza kutumika kama mtaji kwenye benki zetu na hivyo kuwezesha nchi kufanya biashara kubwa na zenye tija kwa taifa na kuwasisitiza wanasiasa kuacha tabia ya kupinga kila kitu kwa sababu tabia hiyo ni umaskini ya kifikra.

“Kuendelea kupinga kila kitu ni umasikini wa kifikra, wanaopinga wanataka wachache waendelee kufaidi, ila tujue wazi kuwa wawekezaji ni sehemu ya uchumi, tushirikiane nao ila sio wa kuwategemea sana kubadilisha maisha yetu, ni lazima tujifunze kushikanama na kujikwamua wenyewe,” alisisitiza Profesa Semboja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma, alisema hatua iliyofanywa na kiongozi huyo wa kampuni ya Barrick, kuja nchini ni ya kiungwana na kwamba timu itakayoundwa kufanya mazungumzo hayo ni vyema ikawa makini, kuzingatia maslahi ya taifa kwanza.

Akizungumzia mwenendo wa wanasiasa nchini kuhusu suala hilo la madini, Profesa Lipumba alisema haileti picha nzuri kuona wapinzani ambao ndio walikuwa mstari wa mbele hapo nyuma, kupinga mikabata mibovu ya madini, leo ndiyo wanakuwa wa kwanza kupinga hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli.

“Sasa unashangaa awali wapinzani ndio tuliokuwa tunapinga mikataba hii mibovu ya madini, tumepata rais ambaye amesikia na kulishughulikia kwa kuchukua hatua, badala ya kumuunga mkono kwa maana tulilipigia kelele siku nyingi, tunapinga tena, huo sio uzalendo,’’ alisema Profesa Lipumba.

Alisema kampuni kama hiyo ni kubwa na ina nguvu kubwa kiuchumi hivyo taifa linapaswa kuungana na kupigania maslahi ya nchi na sio wanasiasa kuwagawa wananchi kwa mambo ambayo hayana tija kwa taifa.

“Sioni msingi wa kupinga jambo hili, tuwe wazalendo kwa nchi yetu kwanza,” alisisitiza Profesha Lipumba. Juni 14, mwaka huu Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa Thornton alifika nchini kwa kutumia ndege binafsi kutoka Canada na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli na kusema wapo tayari kulipa fedha ambazo nchi imepoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha biashara zake hapa nchini.

Katika ripoti ya pili ya kamati iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza harasa za kiuchumi ilibainika kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya Sh trilioni 108 katika kipindi cha miaka 19 kuanzia mwaka 1998 hadi Machi mwaka 2017, kwenye mikataba mibovu ya madini.