Wabunge wasimama dakika moja kutambua kazi anazofanya JPM

WABUNGE hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametumia ujio wa Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Corporation ya Canada, Profesa John Thornton kuwasuta wale waliokuwa wakieleza kuwa Tanzania itashitakiwa kwa hatua inazochukua kulinda madini yake.

Aidha, wabunge hao jana walisimama kwa dakika moja, kumpa heshima Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kukabiliana na wezi wa rasilimali za Taifa. Katika mjadala wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2017/18 bungeni juzi na jana, wabunge hao wamesema ujio wa bosi huyo wa Barrick ni kielelezo kuwa Rais yuko sahihi katika kulinda rasilimali za Taifa na waliokuwa wanasema Tanzania itashitakiwa, wameumbuka.

Baada ya kutoka taarifa katika vyombo vya habari juzi jioni kuwa Rais Magufuli amekutana na Profesa Thornton wa Barrick Corporation yenye hisa nyingi katika Kampuni ya Acacia, wabunge katika michango yao pamoja na jana, waliwanyooshea vidole waliodai Tanzania itashitakiwa.

Mbunge wa Mkuranga, Abdalla Ulega (CCM) alirusha makombora mazito kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akisema amekuwa mtetezi wa mabeberu na sasa ameumbuka kutokana na kuja kwa bosi huyo aliyeahidi kulipa fedha walichota kupitia makinikia katika migodi wanayomiliki nchini.

“Hawa (wapinzani) walijigeuza mawakili wa wezi, sasa wameumbuka. Mzungu kaja na ameahidi kulipa fedha zetu na kuweka kiwanda cha smelter. “Wamepata aibu kubwa na wengine hata viti vyao vya mbele wamehama leo (akimsema Lissu ambaye alikuwa wakati huo amekaa nyuma na kulazimika kuinuka na kwenda mbele katika kiti chake cha kawaida).

Magufuli sio mtu wa mchezo mchezo,” alieleza Ulega. Naye Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli alisema kuja kwa bosi huyo wa Barrick ni kielelezo kuwa Rais yuko sahihi katika kutetea wananchi wanyonge nchini.

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate (CCM), alisema Mungu yupo kazini, na kwamba Rais ameonesha ujasiri mkubwa na ndiyo maana wenye migodi sasa wanahaha. Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Ileje, Janeth Mbene (CCM), alisema, “Wenye macho na masikio wameona na kusikia, wale waliosema tutashitakiwa, badala ya kushitakiwa, wamekuja wenyewe nginjanginja. Rais Magufuli endelee baba.”

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) alisema Rais Magufuli ataipeleka Tanzania kuwa Taifa la uchumi wa kati kwa hatua anazochukua sasa. Aidha, Mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu (CCM), alisema yuko tayari kuisaidia serikali kuonesha jinsi wizi unavyofanyika katika migodi kwani siyo Acacia pekee, wanaoiba rasilimali, bali kampuni nyingi za madini.

Katika mchango wake, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), aliwaomba wabunge wasimame kwa dakika moja na kumpa heshima Rais Magufuli, na wabunge kwa pamoja walisimama na kupiga makofi meza zao kwa heshima ya kazi nzuri ya Rais.

Mbali na hilo, Ngeleja alieleza kufurahishwa na mazungumzo ya Rais na bosi wa Barrick kwamba yataleta kupatikana kwa fedha za Watanzania na sasa kunaelekea kuwa na upatikanaji wa manufaa kwa kila upande.

Hata hivyo, akijibu taarifa ya Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema) kuwa yeye ni mtuhumiwa wa sakata la makinikia, Ngeleja alisema, “Kutuhumiwa siyo kupatikana na hatia mdogo wangu Haonga.

Sisi tunachapa kazi na tunasonga mbele.” Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), alimtaka rais aendelee kupiga kazi na wanamuunga mkono, lakini akawageukia wabunge wa Upinzani akisema wanafanya kazi ya maigizo na kutafuta maisha.

Aliitaka serikali kuchukua hatua pia kwa migodi mingine ukiwamo Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), ambao alidai baada ya kuona rais anasafisha wenzao, waliitwa ili kupewa mradi wa bomba la maji, lakini wamekataa na wanataka kulipwa mamilioni ya fedha za kodi.

Msukuma pia aliwageukia wabunge wenzake waliotajwa katika sakata la makikinia; Ngeleja, Andrew Chenge na Dk Dalaly Kafumu, akisema wanapaswa kushughulikia kwani hawana kinga ya maisha.

Hakuwaacha nyuma wasomi na mawaziri akisema umefika wakati mawaziri wafanyiwe usaili badala ya kuegemea katika vyeti vyao vya kuwa na kiwango cha juu cha elimu kwani uwezo wao wengine ni mdogo.

Kwa upande wao, wabunge wa Upinzani waliendelea kutaka wahusika wa kashfa za makinikia wakiwamo wabunge na mawaziri wa zamani kuchukuliwa hatua. Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) alisema wapinzani hawahusiki na kashfa hiyo kwani mikataba hiyo iliingiwa na Serikali ya CCM.

Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omar (CUF) alisifu bajeti ijayo akieleza kuwa imewalenga wananchi na kuipongeza serikali kwa kubana matumizi, lakini akaitaka ijitahidi katika ukusanyaji mapato.

Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Said Lulida (CUF), alisema wabunge wote bila kujali vyama vyao wanapaswa kutubu na kuwaomba radhi wananchi wa majimbo yao kwa kulifikisha Taifa hapo lilipo.