Chadema: Ulindaji rasilimali za taifa usiishie katika madini pekee

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshauri Rais Dk John Magufuli kuwa dhamira yake ya kulinda rasilimali za Watanzania isiishie katika mikataba ya madini bali mikataba ya sekta zote iwekwe wazi.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji ameyasema hayo leo (Ijumaa) wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo amesema hatua hiyo ya mikataba kuwekwa wazi itasaidia kulinda rasilimali za taifa ambazo ni mali ya Watanzania.

"Dhamira ya Rais Magufuli katika mapambano haya, hasa kuweka uwazi mikataba inayoingiwa kwa siri kati ya serikali na wawekezaji isiishie kwenye mikataba ya madini pekee, sasa tunataka mikataba yote iwekwe hadharani ikiwemo ya sekta ya ujenzi, uuzwaji wa mashirika ya umma," alisema Dk Mashinjii.

Aidha, Chama hicho kimeshauri mabadiliko yoyote yanayotarajiwa kufanyika mbali na kuweka uwazi katika mikataba na kubadili sheria , yanapaswa pia kulenga kufumua hali iliyopo ili kuweka mifumo na taasisi imara zitakazosimamia uwajibikaji na maslahi ya taifa dhidi ya mtu au kikundi cha watu.