Sababu za machifu kumfananisha Rais Magufuli na Nabii Musa

MWENYEKITI wa Machifu Tanzania, Frank Marealle (81) ametaja sababu za kumfananisha Rais John Magufuli na Nabii Musa, akidai wote wanatetea maslahi ya watu wao. ‘’Sisi tupo tangu zamani hatujawahi kuona Rais ambaye amekuwa akiwasikiliza watu wake kama Rais Magufuli…

Namfananisha na Nabii Musa, ingawa Musa aliteuliwa na Mungu na Rais Magufuli amechaguliwa na wananchi,” alisema Chifu Marealle wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana akiwa ameongozana na Chifu wa Wagogo wa Dodoma, Ally Bilingi (74).

Alisema kitendo cha Rais Magufuli kuzuia mchanga kusafirishwa nje ya nchi kinatakiwa kuungwa mkono kwani ni cha kishujaa kwa manufaa ya umma. Aliongeza, ‘’Anachokifanya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu na mimi nikiwa kama Mangi wa Marangu, nampongeza na nitaendelea kumpa ushirikiano wa hali na mali.”

Alisema kutokana na Rais Magufuli kuwa muwazi na kusema hadharani mambo mbalimbali, yaliyokuwa yakifanywa katika kuharibu nchi na ufisadi, ni wajibu wa Watanzania wote kuungana naye.

Marealle ambaye ni Chifu wa Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro, alisema watu wengi walikuwa hawaelewi Rais anataka nini, lakini sasa wanamwelewa kutokana na matendo yake, yanayokwenda na kile anachokimaanisha, kwani amethubutu kuirejesha nchi katika heshima yake.

Chifu Marealle alitawazwa Machi, 2014 akimrithi Chifu Augustino Marealle. Alisema Rais Magufuli amethubutu kikamilifu kuirejesha nchi katika heshima yake hivyo, Watanzania wanatakiwa kujivunia utumishi wake.

Kwa upande wake, Chifu wa Wagogo, Ally Bilingi, alisema Rais Magufuli amemfurahisha kwa kuifuta Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kupeleka Makuu ya Nchi mkoani Dodoma kutoka Dar es Salaam, hivyo Rais anapaswa kuungwa mkono kwa anayoyafanya.

Alisema amefurahishwa kwa kuwa yeye akiwa Chifu wa Wagogo, wananchi wake walinyanyaswa na Mamlaka hiyo kwa kuondolewa kwa nguvu kwenye maeneo yao bila kulipwa fidia.

“Rais Magufuli ameweza, tukumbuke hii ni miaka miwili tu, bado ana miaka mingine mitano, nina uhakika atatufikisha mbali,’’ alisema. Chifu Bilingi ni mjukuu wa Chifu wa Wagogo, Salehe Bilingi, aliyeishi eneo la Makulu mjini Dodoma na baada ya kufariki, alimuachia mikoba Chifu Ngalya Bilingi, ambaye naye alifariki mwaka 1972.