‘Udhalilishaji husababisha magonjwa ya akili’

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) amewataka wazazi kuungana kupiga vita dawa za kulevya na udhalilishaji, kwa kuwa mambo hayo husababisha magonjwa ya akili.

Kwa msingi huo, Makamu wa Rais amewataka wazazi na jamii, kufuatilia mienendo ya watoto kwa kuwa watoto na vijana wanashawishiana kuanzia shuleni, hivyo wazazi wanapaswa kuwa imara kuokoa kizazi.

Samia alisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, ambayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, yalifanyika katika viwanja vya michezo vya Shule ya Msingi Kinyerezi Manispaa ya Ilala.

Alisema magonjwa ya akili ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, yanayowaathiri watu wazima, watoto na vijana. “Vitendo vya udhalilishaji watoto vimekuwa kwa kasi, hivyo wazazi unapomuona mtoto amebadilika, toeni taarifa kwa walimu wawafuatilie.

Pia watoto wenyewe mnatakiwa kulindana unapomuona mwenzako anadhalilika toeni taarifa kwa askari au mwalimu na msikubali kufanyiwa vitendo vya uzalilishaji,” alisema Samia.

Alisema Taifa linatumia fedha nyingi, kuwatunza na kuwanusuru watoto wanaougua magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza, kwani vifo vyao hupunguza nguvu kazi ya Taifa na kupunguza uzalishaji.

Alisema takwimu za mwaka 2014/15, zinaonesha kuwa asilimia 90 ya hospitali hutoa huduma za kisukari na asilimia 60 huduma za moyo, hivyo inadhihirisha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Pia alifafanua kuwa idadi kubwa ya watoto, hufanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kwamba taasisi hiyo imesaidia kuokoa mabilioni ya shilingi ya watu kutibiwa nje.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala alisema magonjwa yasiyoambukiza, husababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kulimbikiza nishati lishe.

Alisema mfumo wa maisha pia unachangia magonjwa hayo, ikiwemo matumizi ya magari na pikipiki hata sehemu yenye umbali mdogo na matumizi ya teknolojia, ikiwemo kompyuta hufanya watu wakae muda mrefu bila kushughulisha mwili.

Mkurugenzi wa Taasisi ya CCP Medicine, Dk Frank Manase alisema walianza upimaji huo kwa siku nne kabla ya jana, ambapo watoto 1,500 walifanyiwa uchunguzi na wengine walipatiwa rufaa.

Dk Manase alisema katika uchunguzi huo, wamegundua wapo watoto ambao hawawezi kuongea, lakini wazazi hawafahamu kama wana magonjwa ya akili. Wengine hawajui kusoma kwa sababu ya nta nyingi masikioni, hivyo hawasikii na magonjwa ya moyo.

“Magonjwa yasiyoambukiza husababisha maumivu ya kimwili, kiakili na kidogo kwa Watanzania na familia zinaporomoka kiuchumi kwa sababu ya magonjwa sugu,” alisema Dk Manase.