Stamico yaanza kuchimba makaa Kiwira

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza kuchimba makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira mkoani Mbeya na katika mwaka huu wa fedha, tani 500 zimeshachimbwa. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Mwanjelwa (CCM).

Mwanjelwa alitaka kujua kauli ya serikali kuhusu kusimamishwa kwa uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira. “Pia kampuni mbili zimeingia ubia katika kuchimba madini hayo na katika mwaka wa fedha 2018/19 tani 1,000 zitachimbwa,” alisema.

Akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Oliver Semuguruka (CCM) aliyetaka kujua wananchi wa Bugarama, Ngara watanufaika vipi na uwepo wa rasilimali ya Kabanga Nickel. Dk Kalemani alisema mgodi huo, unatajiwa kutoa ajira 1,355 wakati wa ujenzi na ajira 800 wakati wa uzalishaji.

“Mradi utakapoanza wananchi wa maeneo ya Bugarama watanufakia kwa kupata ajira, kuuzia mgodi bidhaa na malipo ya utoaji huduma kwenye halmashauri yao na kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa na mgodi kwenye afya, maji, elimu na miundombinu.

Alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea kufanya utafiti wa kina ili kubaini kama mradi huo unaweza kuendelezwa kwa faida. Kampuni ya Kabanga Nickel inamiliki mradi wa utafutaji madini ya nickel katika eneo la Kabanga chini ya leseni namba RL 0001/2009 iliyotolewa Mei 2, 2009.

“Lakini katika mwaka 2010 bei ya madini ya nickel ilishuka ghafla kutoka dola za Marekani 11 kwa pauni na kufikia wastani wa dola za Marekani nne kwa pauni mwaka 2014,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, kampuni hiyo inatarajia kuendeleza shughuli za uchimbaji mara baada ya bei ya nickel kuimarika kwani hadi kufikia Aprili 4, mwaka huu, bado bei ya nickel ni dola 4.45 kwa pauni, ikilinganisha na dola 11 kwa paundi wakati wa upembuzi yakinifu.