Wizara yakusanya tril. 1.4/- kodi ya ardhi

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kanda ya Kati, imevuka malengo iliyopangiwa baada ya kusanya Sh trilioni 1.43 sawa na asilimia 204 ya Makusanyo ya Kodi ya pango la ardhi.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Kanda ya Kati Dodoma, Hezekiel Kitillya alisema kuwa tathimini iliyofanyika mpaka Mei 31 mwaka huu, inaonesha kuwa malengo ya makusanyo yaliyokuwa yamepangwa na wizara hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17. Alisema mpaka Juni 30, mwaka huu walikuwa wamekusanya kodi ya Sh bilioni 111.77, ambapo kati ya kanda nane za ardhi zilizopo nchini, kanda ya kati ilipangiwa kukusanya Sh milioni 700.

Vilevile, baadhi ya halmashauri zilivuka malengo ya makusanyo zilizowekewa, kama vile Manispaa ya Dodoma, malengo yalikuwa Sh milioni 200 na makusanyo yakawa Sh milioni 678.8.

Manispaa ya Singida, malengo yalikuwa Sh milioni 200 na makusanyo yakawa Sh milioni 308.39 na Halmashauri ya Manyoni, malengo yalikuwa Sh milioni 100 na makusanyo yakawa Sh milioni 117.2. Pia Halmashauri nyingine za Wilaya ya Itigi, Chamwino, Bahi nazo zilivuka malengo na nyingine zilizobaki zikikaribia kufikia malengo. Akieleza moja ya mkakati muhimu ambao umewezesha kanda yake kuvuka malengo ni pamoja na kusambaza hati za madai. Akizungumzia moja ya changamoto kuu inayokabili makusanyo, alisema ni wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu tofauti ya kodi ya ardhi na kodi ya majengo, ambapo wananchi wengi hudhani wakishajenga nyumba na kuanza kulipa kodi ya jengo, hawapaswi tena kulipa kodi ya pango la ardhi. Kanda ya kati inahudumia mikoa miwili Dodoma na Singida yenye jumla ya halmashauri 15.