Serikali kupunguza watoto wa mtaani kwa asilimia 50

SERIKALI itaendelea kuwawekea mazingira bora watoto kukua kiafya, kielimu na kimaadili na kuwaondolea vikwazo katika maendeleo ikiwemo kuhakikisha kuwa idadi ya watoto 35,916 wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanapungua kwa asilimia 50.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Alisema Tanzania kuna watoto wanaokadiriwa kufikia asilimia 50.1 ya jamii nzima na watoto hao wanahitaji kupatiwa haki za msingi ikiwemo elimu, afya, ulinzi na malezi bora bila ubaguzi.

Dk Kigwangalla alisema serikali imekuwa ikiweka mazingira bora ya watoto ili waweze kukua kiafya, kielimu na kimaadili kwa kuwaondolea vikwazo katika maendeleo yao. Alisema mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano unatarajia kumaliza tatizo la ukatili kwa watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 20121/2022.

Alisema malengo hayo yatafikiwa kwa kuhakikisha kuwa idadi ya watoto 35,916 wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanapungua kwa asilimia 50. Pia kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka asilimia 29 hadi asilimia tisa, kuimarisha huduma ya elimu kwa watoto wa kike wanaotoka katika familia maskini kutoka asilimia 23.4 hadi asilimia 53.4 Alitaja juhudi nyingine ambazo serikali imefanya katika kuendeleza haki na ustawi wa watoto hapa nchini ni pamoja na kutoa elimu ya malezi na makuzi ya mtoto katika ngazi ya familia, shule katika halmashauri 74 ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto wa kike.

Pia kuanzishwa kwa timu ya ulinzi wa mtoto katika halmashauri za wilaya 63 ili kuboresha utoaji huduma stahiki kwa watoto walioathiriwa na vitendo vya ukatili. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la watoto wa Tanzania, Joel Festo, aliwataka watoto kusoma kwa bidii kwani wakati Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda itahitaji wataalam wengi.